1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Zimbabwe yatangaza Agosti 23 kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu

Iddi Ssessanga
1 Juni 2023

Zimbabwe imetangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, na kuibua tena matarajio ya mpambano kati ya rais alieko madarakani Emmerson Mnangagwa na kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa. Wachambuzi watabiri mchuano mkali.

https://p.dw.com/p/4S4vM
Simbabwe | Präsident Emmerson Mnangagwa
Picha: Jekesai Njikizana/AFP/Getty Images

Rais Emmerson Mnangagwamwenye umri wa miaka 80, aliyechukuwa nafasi ya Robert Mugabe mwaka 2017 baada ya mapinduzi yalioongozwa na jeshi, anaongoza chama tawala cha ZANU-PF, kilichopo madarakani tangu uhuru mwaka 1980.

Mpinzani mkuu wa Mnangagwa ni Nelson Chamisa, wakili na mchungaji mwenye umri wa miaka 45, anaeongoza chama kilichoundwa hivi karibuni cha Muungano wa Raia kwa ajili ya Mabadiliko, CCC, na ambaye alishindwa kwa tofauti ndogo sana na Mnangagwa mwaka 2018.

Soma pia: Zimbabwe yatangaza 23 Agosti kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu

Wachambuzi wanajiandaa kwa kura yenye ushindani mkali, katika taifa ambako hali ya kutoridhika kutokana na umaskini uliokithiri, ukatikaji wa mara kwa mara wa umeme na uhaba mwingine vimekita mizizi. Mashirika ya haki za binadamu na vyama vya upinzani yamelalamika kuhusu ukandamizaji kuelekea uchaguzi huo.

Hatua muhimu kwa mustakabali wa taifa

Baada ya kutangazwa kwa tarehe ya uchaguzi, chama cha CCC kiliwahimiza wafuasi wake kujiandikisha ili kushiriki zoezi la upingaji kura, kikisema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter, kwamba hiyo ni hatua muhimu katika kushiriki kwao kujenga mustakabali wa taifa lao.

Simbabwe | Kundgebung der Opposition in Simbabwe
Mgombea wa chama cha Muungano wa Kiraia kwa ajili ya Mabadiliko, CCC, Nelson Chamisa.Picha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP/picture alliance

Mnamo mwaka 2018, Mnangagwa aliepewa jina la utani la "mamba" kutokana na umahiri wake wa kisiasa, alishinda uchaguzi uliogubikwa na vurugu kwa asilimia 50.8 ya kura.

Matokeo hayo yalipingwa kama udanganyifu na Chamisa, ambaye wakati huo aliongoza Muungano wa Vuguvugu la Mabadiliko ya Kidemokrasia, MDC-Alliance.

Chama tawala pia kilishinda viti 145 kati ya 210 vilivyowaniwa katika bunge la taifa, huku muungano wa MDC ukipata viti 63, na viti viwili vikichukuliwa na wagombea binafsi.

Soma pia:Zimbabwe yawaachia wafungwa kupunguza msongamano magerezani 

Viti vingine 60 vinahifadhiwa kwa ajili ya wanawake wanaoteuliwa kupitia mfumo wa orodha ya vyama kutegemea na idadi ya kura kilizopata chama husika.

Baraza la Seneti linaundwa na wajumbe 80 ambapo 60 huteuliwa kupitia mfumo wa uwakilishi wa uwiano, machifu 18 wa jadi ambao kimsingi ni watiifu kwa chama cha ZANU-PF na wawakilishi wawili wa watu wenye ulemavu.

Mlima mrefu kwa Chamisa kumshinda Mnangagwa

Wachambuzi wanasema Chamisa anakabiliwa na mapambano makali kumshinda Mnangagwa. Wakosoaji wanaituhumu serikali kutumia mahakama kuwaweka kando wapinzani na wanasema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukamataji wa holela na ukandamizaji wa mashirika ya kutetea haki.

Simbabwe | Wahllokal in Harare
Gazeti rasmi la serikali ya Zimbabwe limetangaza Agosti 23 kuwa siku ya uchaguzi wa rais, bunge na serikali za mitaa.Picha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP Photo/picture alliance

Baadhi wameibua pia hofu ya kasoro za upigaji kura. Mapema wiki hii muungano wa CCC ulilalamika baada ya wapigakura wengi, wakiwemo baadhi ya wanasiasa wandamizi, kusema walikuwa wameondolewa au kuwekwa ndivyo sivyo kwenye daftari la wapigakura.

Tafadzwa Sambiri, msemaji wa Team Pachedu, ambalo ni kundi la harakati, aliliambia shirika la habari la AFP, kwamba taifa hilo halikuwa tayari kwenda kwenye uchaguzi, akisema ni jambo moja kupanga tarehe ya uchaguzi, na jambo jengine kuendesha uchaguzi huru na wa haki.

Soma pia: Je Afrika yaweza kuimarisha demokrasia mwaka 2023?

Zimbabwe, nchi isiyo na bandari iliyoko kati ya Msumbiji, Afrika Kusini, Botswana na Zambia, ina wakaazi wapatao milioni 15 kwa mujibu sensa ya karibuni. Kwa muda mrefu imekabiliana na mfumuko mkubwa wa bei, uliopindukia katika wiki za karibuni, huku wachambuzi wakikadiria kuwa kwenye asilimia 700, juu kabisaa ya kiwango rasi cha asilimia 280.

Nchi hiyo inaorodheshwa katika nafasi ya 137 kati ya mataifa 180 katika faharasi ya uhuru ya shirika la waandishi habari wasio na mipaka, na ya 157 kati ya mataifa ya 180 kwenye faharasi ya rushwa ya shirika la Transparency International.

Chanzo: AFP