1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck awasili Ukraine

18 Aprili 2024

Waziri Robert Habeck amewasili Kiev leo katika ziara inayolenga kuangazia mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine, misaada ya dharura na uimarishaji wa uchumi wa nchi hiyo

https://p.dw.com/p/4ev7Y
 Habeck Ukraine
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amewasili kwa ziara maalum mjini Kiev, Ukraine hii leo Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

      
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amewasili Kiev leo katika ziara yake inayolenga kuangazia mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine, misaada ya dharura na uimarishaji wa uchumi wa nchi hiyo, wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi saba zilizoimarika kiviwanda duniani, G7, wapo nchini Italia kujadili namna ya kuisaidia Ukraine kwenye vita vyake dhidi ya Urusi.

Soma zaidi. Zelensky atoa wito wa mshikamano baada ya shambulio la Urusi

Ziara ya Habeck inakuja wakati Ujerumani ikijiandaa kwa mkutano mjini Berlin mnamo Juni 11 na 12, ambapo Kansela Olaf Scholz na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky watashiriki kwa pamoja kuandaa mkutano huo wa kimataifa wa kusaidia kuijenga upya Ukraine baada ya vita.

Alipowasili mjini Kiev, Waziri huyo amesema kwamba Ukraine inahitaji msaada wa kila namna ili iweze kuendelea na mapambano yake ya dhidi ya uvamizi wa Urusi. 

Habeck/ Ukraine
ziara ya Habeck inalenga kuangazia mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine, misaada ya dharura na uimarishaji wa uchumi wa nchi hiyoPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Soma zaidi. G7 yalaani mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel

Mashambulizi ya Urusi ya droni na makombora nchini Ukraine yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, yakilenga miundo mbinu ya nishati na kusababisha kukatika kwa umeme katika makazi ya watu na viwandani, wakati ambapo Ukraine ikizidi kupungukiwa na uwezo wa kujilinda angani.

Waokoaji: Watu 18 wamepoteza maisha

Waokoaji wa Ukraine katika mji wa kihistoria wa mji wa Chernigiv wamesema mashambulizi ya makombora ya hapo jana yamewaua watu 18 huku wengine 77 wakiwemo watoto wakijeruhiwa.

Mashambulizi hayo yaliyotokea kaskazini mwa Ukraine yameongeza mwito mpya kwa washirika wa nchi hiyo wa kusaidia kuimarisha mifumo ya ulinzi wake wa anga.

Kwa upande mwingine,Mawaziri wa Mambo ya Nje wa mataifa ya G7 wapo nchini Italia kujadili namna ya kuisaidia Ukraine huku suala la ulinzi wa anga likiwa ndio kitovu cha mazungumzo hayo.

Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anashiriki mkutano wa G7 unaofanyika nchini Italia wa kujadili namna ya kuisaidia UkrainePicha: Christophe Ena/dpa/AP/picture alliance

Soma zaidi. Naibu Kansela wa Ujerumani afanya ziara ya ghafla Ukraine

Akiwa kwenye mkutano huo, Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amesema ana matumaini kuwa kwa sasa wabunge wa Marekani wataafikiana katika kuisaidia Ukraine kuhusiana na msaada wake uliokwamishwa na wabunge wa Republican.

 "Katika nyakati hizi za msukosuko, Kuna ishara kutoka kwa chama cha Republican nchini Marekani kwamba kitaunga mkono msaada kwa Ukraine. Inawezekana, Tumefanya kampeni kubwa kwa hili, Kansela wa Ujerumani alikuwa katika bunge la Marekani na mimi nilikuwa huko pia."amesema Baerbock

Hapo jana kiongozi wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi alitangaza kupiga kura ya kuunga mkono mfuko mpya wa msaada wa kijeshi ambao unajumuisha dola bilioni 61 za msaada kwa Ukraine.

Vyanzo : DPA, AFP; Reuters
Mwandishi: Suleman Mwiru