1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kyiv yaidhinisha mswada wa kuwaajiri watu jeshini

Bruce Amani
11 Aprili 2024

Wabunge nchini Ukraine wameidhinisha muswada wa kuwaajiri watu jeshini ambao umezusha hasira baada ya kuondolewa vipengele vilivyoruhusu askari waliohudumu kwa muda mrefu kuwachishwa kazi.

https://p.dw.com/p/4efVi
Wanajeshi wa Ukraine
Baadhi ya wanajeshi wa Ukraine wakiwa mjini DonetskPicha: Diego Herrera Carcedo/Anadolu/picture alliance

Huku wakikabiliwa na shinikizo kutoka kwa maafisa wa jeshi, wabunge waliondoa kipengele kwenye mswada huo ambacho kingewaruhusu askari walioko vitani kwa zaidi ya miezi 36 kurejea nyumbani.

Mswada huo unaohitaji kutiwa saini na Rais Volodymir Zelensky ili kuwa sheria, utaongeza adhabu kwa watakaokwepa kuajiriwa jeshini.

Zelensky: Ukraine imepata mafanikio katika utengenezaji wa makombora

Kyiv imekuwa na changamoto kwenye uwanja wa mapambano kwa miezi kadhaa, ikidhoofishwa na msaada unaohitajika kwa dharura wa Marekani ambao umezuiwa na Bunge, na uhaba wa askari na silaha.

Urusi ilifanya mashambulizi ya angani ya usiku kucha katika maeneo matano ya Ukraine, na kuwauwa watu wanne katika mji wa kusini wa Mykolaiv. Mashambulizi hayo yaliharibu kabisa kituo muhimu cha umeme karibu na Kyiv.

Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Lithuania, Rais Zelensky amezihimiza nchi za Magharibi kutoyafumbia macho mashambulizi ya angani ya Urusi na kuipa Ukraine mifumo zaidi ya ulinzi wa angani.