1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mabadiliko ya tabianchi yasababisha joto kali

Tatu Karema
6 Septemba 2023

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mawimbi makali zaidi na ya mara kwa mara ya joto, ambayo hugeuka na kusababisha uchafuzi wa mazingira, unaotishia afya ya binadamu na viumbe hai

https://p.dw.com/p/4W214
Quallen Mittelmeer
Picha: JOSE JORDAN/AFP

Katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu ubora wa hewa na hali ya hewa, shirika la hali ya hewa duniani  (WMO) limesema kuwa joto kali linaweza pia kuchochea michakato mingine mingi ya kemikali ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu. Katika taarifa, mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema mawimbi ya joto yanaharibu ubora wa hewa, na kuwa na athari mbaya kwa afya ya binadamu, mifumo ya ikolojia, kilimo na maisha ya kila siku.

Uchafuzi kutoka vyanzo kama vile gesi chafu za magari na viwandani ni tishio kubwa la nje kwa afya ya umma

Utafiti mpya wa taasisi ya sera ya nishati katika chuo kikuu cha Chicago, umeonyesha kuwa uchafuzi wa chembe chembe kutoka kwa vyanzo kama vile gesi chafu za magari na viwandani, mchanga na moto wa nyika ni tishio kubwa zaidi la nje kwa afya ya umma ulimwenguni kote. Taalas amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi na ubora wa hewa haviwezi kushughulikiwa tofauti na kwamba vinaambatana na hivxo lazima kushughulikiwa kwa pamoja ili kuvunja utaratibu huo.

Soma pia: Marekani yakabiliwa na kitisho cha wimbi la joto kali

Wakati ripoti hiyo ya leo ikizingatia takwimu za mwaka 2022, Taalas ametahadharisha kwamba katika misingi ya viwango vya joto, kile kinachoshuhudiwa mwaka huu wa 2023 ni kiwango cha juu zaidi.

Mwaka 2023 huenda ukawa wa joto zaidi

Mvua kubwa Kaskazini mwa India yasababisha kufuta kwa mto Yamuna
Mvua kubwa Kaskazini mwa IndiaPicha: Ab Rauoof Ganie/DW

Jumatano (6.09.2023) Mpango wa Uangalizi wa Dunia wa Umoja wa Ulaya, umesema kuwa mwaka wa 2023 huenda ukawa na kiwango cha joto zaidi katika historia ya binadamu baada ya miezi mitatu iliyopita kurekodi viwango vya joto vya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa. Hii inaweza kuwa habari mbaya kwa ubora wa hewa. 

Soma pia: Jitihada za kupunguza joto ulimwenguni

WMO imesema kuwa ubora wa hewa na hali ya hewa vinaingiliana kwasababu spishi za kemikali zinazoathiri zote mbili zimeunganishwa.  Viini vinavyohusika katika mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa ubora wa hewa mara nyingi hutoka kwa vyanzo sawa, na mabadiliko katika kiini kimoja husababisha mabadiliko katika kingine.

Mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mawimbi makali na ya mara kwa mara ya joto

WMO imeelezea kwa mfano jinsi mwako wa nishati ya visukuku unavyotoa hewa chafu ya kaboni na nitrogen dioksid kwenye hewa. Wakati huo huo, watafiti wanakubaliana kwa kiasi kikubwa kwamba mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mawimbi makali na ya mara kwa mara ya joto na kuchangia kuongezeka kwa athari ya mioto mibaya zaidi ya nyika.

Soma pia:Maelfu ya wanafunzi waandamana kutetea mazingira

Lorenzo Labrador, mtafiti mmoja wa WMO katika mtandao wa Global Atmosphere Watch uliotayarisha ripoti hii ya leo, amesema mawimbi ya joto na mioto ya nyika yanaingiliana kwa karibu. Labrador amesisitiza kuwa bado ni mapema kusema iwapo mwaka 2023 utathibitisha kuwa mbaya zaidi katika uchafuzi wa hewa ikilinganishwa na mwaka jana.