1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yatibua njama ya kumuua waziri Itamar Ben Gvir

Tatu Karema
4 Aprili 2024

Idara ya usalama ya Israel imesema leo kuwa imetibua njama ya kumuua waziri wa usalama wa kitaifa wa mrengo mkali wa kulia Itamar Ben Gvir

https://p.dw.com/p/4eRGx
Waziri wa usalama wa kitaifa wa Israel Itamar Ben Gvir akizungumza wakati wa kongamano la ujenzi wa makazi zaidi ya kiyahudi katika ukanda wa Gaza mnamo Januari 28, 2024
Waziri wa usalama wa kitaifa wa Israel Itamar Ben GvirPicha: Debbie Hill/UPI Photo/IMAGO

Watu 11 wanaowajumuisha raia saba wenye uraia pacha wa Palestina na Israeli wamekamatwa katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na polisi na jeshi la Israel. Haya ni kulingana na idara ya usalama ya Israel, Shin Bet.

Shambulizi lilimlenga waziri wa usalama wa kitaifa Itamar Ben Gvir

Taarifa hiyo imesema kuwa Shin Bet, ilisambaratisha kundi la kigaidi lililokuwa linapanga mashambulizi nchini Israel, hasa dhidi ya Ben Gvir, takriban miezi sita baada ya kuzuka kwa vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza.

Soma pia:Israel yasema shambulizi lililowauwa wafanyakazi wa misaada lilikuwa "kosa kubwa"

Taasisi hiyo imeendelea kusema kuwa washukiwa hao walikuwa wamepanga kumuua Ben Gvir kwa roketi na pia kushambulia kambi za kijeshi, uwanja wa ndege wa Ben Gurion na ofisi za serikali mjini Jerusalem.

Mashambulizi mengine mawili pia yatibuliwa

Shin Bet imeongeza kuwa washukiwa 10 walishtakiwa leo katika mahakama moja ya Beersheva Kusini mwa nchi hiyo. Polisi na Shin Bet pia wamesema kuwa wametibua mashambulizi mawili yaliyokuwa yamepangwa na wafuasi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, Mashariki mwa Jerusalem.

WCK yasema Israel ilidhamiria kuwalenga maafisa wake

Afisa mkuu mtendaji wa shirika la misaada la World Central Kitchen, WCK, Erin Gore na mwenza wake Javier Garcia, wamesema kuwa shambulizi dhidi ya msafara wao wa msaada lilikuwa la kijeshi lililolenga magari yao matatu.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiongoza kikao cha baraza la mawaziri kati wizara ya ulinzi mjini Tel Aviv mnamo Januari 7, 2024
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/AFP/Getty Images

Katika taarifa ya pamoja, wamesema magari yote matatu yalikuwa yamewabeba raia na kuwekwa nembo ya shirika hilo huku msafara huo ukizingatia maagizo ya mamlaka yaIsrael iliyokuwa inafahamu kuhusu mipango yao, njia za kutumia na ujumbe wao wa kibinadamu.

Vifo vya wafanyakazi wa WCK vyaibua shtuma za kimataifa

Vifo vya wafanyakazi saba wa shirika hilo vilivyosababishwa na shambulizi hilo la Israel, vimeibua shutuma kali za kimataifa wakiwemo washirika wa Israel.

Rais wa Poland Andrzej Duda ambaye raia wake mmoja aliuawa katika shambulizi hilo amesema kuwa hana shaka kwamba Israel inapaswa kulipia fidia kwa familia ya raia wake aliyeuawa katika ukanda wa Gaza na kwamba inapaswa kutolewa kwa uadilfu na haki bila ya kuzingatia sababu ya tukio hilo.

Soma pia:Kwa muda gani Netanyahu ataendelea kubakia tena madarakani?

Hapo jana, mwanzilishi wa WCK José Andrés ambaye ni mpishi maarufu mwenye makazi yake nchini Marekani, alikiambia kituo cha habari cha Israel, Channel 12 kwamba shambulizi hilo la anga lilikuwa la moja kwa moja dhidi ya wafanyakazi hao wa msaada na kwamba vikosi vya Israelivilikusudia kufanya hivyo.

Haya yanajiri wakati ambapo rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa leo kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Netanyahu.