1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya shambulio katika ardhi ya Iran

Saumu Mwasimba
19 Aprili 2024

Israel imefanya shambulio katika ardhi ya Iran leo Ijumaa (19 Aprili) siku kadhaa baada ya Iran kuishambulia kwa makombora na droni nchi hiyo katika hatua ya kulipiza kisasi.

https://p.dw.com/p/4exhm
Kombobild Iran-Israel Flaggen
Bendera za Iran na IsraelPicha: H. Tschanz-Hofmann/IMAGO

Shirika la habari la Iran limeripoti juu ya kutokea miripuko katika mkoa wa kati wa Isfaham leo Ijumaa.

Vyombo vya habari nchini Marekani vikinukuu taarifa za maafisa wa nchi hiyo vimesema kwamba Israel imefanya mashambulizi dhidi ya Iran.

Soma zaidi: Hofu yaongezeka Mashariki ya Kati baada ya Israel kuishambulia Iran

Jumuiya ya kimataifa imetoa kauli za tahadhari kwa pande zote mbili kujizuia kutanua mgogoro huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, amesema watalijadili suala hilo katika mazungumzo na wenzake wa Kundi la Nchi Tajiri kiviwanda G7 wanaokutana kwa siku ya mwisho katika mji wa Capri.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Melanie Joly, kupitia ukurasa wa X ameandika ujumbe akisema wanafuatilia kwa karibu juu ya ripoti hiyo.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pia ametowa mwito wa kuepusha kutanuka kwa mgogoro katika Mashariki ya Kati.