1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya mashambulizi dhidi ya Iran

19 Aprili 2024

Taarifa zinaeleza kuwa Israel imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran. Miito imetolewa kwa Israel na Iran kujizuia na hatua zozote zitakazopelekea mzozo huo kutanuka katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4exiJ
Iran | Wanajeshi wa Iran wakilinda miundombinu ya nyuklia huko Isfahan
Maafisa wa kijeshi wakilinda kituo cha nyuklia katika eneo la Zardanjan huko Isfahan, Iran, Aprili 19, 2024Picha: West Asia News Agency/REUTERS

Vyanzo mbalimbali vinaarifu kuwa leo Ijumaa, Israel imefanya shambulio la kulipiza kisasi katika ardhi ya Iran. Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kwamba  milipuko ilisikika katika mji wa katikati mwa Iran wa Isfahan , lakini afisa mmoja Tehran ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba milipuko hiyo ilisababishwa na mifumo ya ulinzi wa anga ambayo ilifanikiwa kudungua droni tatu.

Viongozi wa Israel na hata jeshi la nchi hiyo hawajazungumza chochote kuhusu taarifa hii. Afisa mwandamizi wa Iran ameiambia Reuters  kuwa nchi hiyo haina mpango wa kujibu mara moja shambulio hilo, ambalo taarifa kutoka Tehran zinasema halikuwa na madhara makubwa.

Iran: Luteka ya kijeshi huko Isfahan
Kombora likifyetuliwa wakati wa luteka ya kijeshi huko Isfahan: 27.10.2023Picha: Iranian Army Office/ZUMA Wire/IMAGO Images

Chanzo kinachofuatilia mzozo huo kimeeleza kuwa Marekani ilipokea taarifa kabla ya Israel kufanya shambulio hilo, ambalo linajiri siku chache baada ya Iran kuendesha mashambulizi ya droni na makombora ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel.

Hata hivyo, Shirika la Kimataifa la kudhibiti Nishati ya Atomiki (IAEA) limesema shambulio hilo halijasababisha uharibifu wowote katika miundombinu ya nyuklia ya Iran na kukumbusha kwamba maeneo yenye miundombinu ya nyuklia haipaswi kulengwa katika mizozo ya kijeshi.

Jumuiya ya Kimataifa yatoa wito wa kuzuia kutanuka kwa mzozo  

Mataifa mbalimbali yamezitolea wito Israel na Iran kutochukua hatua zitakazo litumbukiza kwenye vita eneo zima la Mashariki ya Kati. Oman, ambayo imekuwa mpatanishi wa muda mrefu kati ya Tehran na Mataifa ya Magharibi, imelaani "shambulio la Israel" dhidi ya Iran.  Kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda G7  linalozijumuisha Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Japan na Canada limetoa wito wa kutochochea mivutano katika eneo hilo, wito uliotolewa na nchi na taasisi nyingine duniani. Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, amesema:

Brussels | Ursula von der Leyen | Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Kenzo Tribouillard/dpa/Pool AFP/AP/picture alliance

"Tunapaswa kufanya kila liwezekanalo ili pande zote zizuie kutanuka kwa mzozo katika eneo hilo. Tumeshuhudia mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani na makombora karibu 300 yaliyoendeshwa na Iran dhidi ya Israel. Ni muhimu kabisa kwamba eneo hilo lisalie kuwa tulivu na kila upande ujiepushe na kuchukua hatua zaidi."

Soma pia: Kwanini Iran na Israel ni maadui?

Australia imewataka raia wake kuondoka Israel na katika maeneo ya Palestina, ikisema kuna tishio kubwa ya kutokea mashambulizi ya kulipiza kisasi au hata mashambulizi ya kigaidi. Shirika la ndege la FlyDubai limefuta safari zake kuelekea Iran.

Kumekuwa na hofu kwamba eneo zima la Mashariki ya Kati linaweza kutumbukia katika vita kamili. Wiki hii, Rais wa Iran Ebrahim Raisi aliionya Israel kwamba watajibu vikali mashambulizi yoyote katika ardhi yake, huku Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisema kwamba eneo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na hatari kubwa.

(Vyanzo: Mashirika)