1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky azuru makao makuu ya NATO na kuomba msaada zaidi

Sylvia Mwehozi
11 Oktoba 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewatolea wito washirika wake wa jumuiya ya kujihami ya NATO kuongeza kasi ya usambazaji silaha kuelekea msimu wa baridi, wakati alipofanya ziara yake ya kwanza mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/4XOUa
Ubelgiji| NATO | Stoltenberg na Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg Picha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Zelensky ametoa wito wa kupatiwa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga, makombora ya masafa marefu na silaha nyinginezo, katikati mwa shambulio la kundi la wanamgambo la Hamas dhidi ya Isreal, akihofia kwamba linaweza kudhoofisha juhudi za mshirika wake mkuu ambaye ni Marekani za kuipatia silaha Ukraine. Akizungumza na vyombo vya habari sambamba na katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg kabla ya kukutana na mawaziri wa ulinzi wa NATO,  Rais Zelensky alisema mkazo mkubwa kwa hivi sasa ni namna nchi hiyo itakavyoweza kuhimili mashambulizi ya Urusi katika msimu ujao wa baridi.

Soma pia: Zelensky atoa mwito wa umoja kwa nchi za NATO

"Vipaumbele vya Ukraine ni namna ya kujilinda, jinsi gani tutaweza kuishi wakati wa msimu wa baridi ujao, hilo ni jambo kubwa kwetu. Moja ya changamoto kubwa ni kwamba itakuwaje!. Lakini hata hivyo tunajiandaa, tuko tayari. Sasa tunahitaji msaada ziaidi kutoka kwa viongozi," alisema Zelensky.

Ukraine, Awdijiwka
Askari wa Ukraine karibu na mji wa Avdiivka mwezi JuniPicha: Genya Savilov/AFP/Getty Images

Mawaziri wa ulinzi wa NATO wanakutana mjini Brussels kulijadili suala la usambazaji wa silaha, huku mkazo mkubwa ukiwa ni namna ya kuisaidia Kyiv kuendeleza mashambulizi na kuipatia mifumo ya ulinzi wa anga ili iweze kujilinda na mashambulizi yanayotarajiwa ya majira ya baridi kutoka kwa Urusi. Zelensky ameelezea wasiwasi kwamba mzozo uliozuka huko Israel  unaweza kuathiri vita vinavyoendelea nchini mwake kwa washirika kuelekeza nguvu katika mzozo wa Israel.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesisitiza dhamira ya muungano huo kuendelea kuisaidia Ukraine. Mawaziri wa NATO pia watajadili athari ya vita vya Moscow kwa muungano huo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha tena uwezo wa ulinzi katika nchi za NATO zilizo karibu na Urusi au mshirika wake Belarus. Ajenda nyingine ni ushiriki wa NATO katika mzozo wa Kosovo ambapo uwepo wa wanajeshi wake umeongezeka hivi karibuni baada ya mvutano kati ya Kosovo na Serbia, na Iraq.

Wakati mkutano huo ukifanyika Brussels, Urusi imeusogelea uwanja wa mapambano kwenye mji wa Avdiivka mashariki mwa Ukraine, huku Kyiv ikionya kwamba Moscow inazidisha mashambulizi katika juhudi za kuuzingira mji huo kikamilifu. Maafisa katika mji huo wamelieleza shirika la habari la AFP kwamba Moscow imefanya shambulizi la anga na wanafyatua risasi bila kukoma.

Mji wa Avdiivka washambuliwa: Watu 1,800 tu wasalia Avdiivka Ukraine

Avdiivka ni mji wa kiviwanda ambao kabla ya vita ulikuwa na takribani wakaazi 31,000 na sasa waliobaki wanakadiriwa kuwa raia 2,000. Mji huo ni muhimu na wa kimkakati kwa Kyiv, ulioko kaskazini mwa mji wa Donetsk unaodhibitiwa na Moscow ambao ulikamatwa na vikosi vya wanaotaka kujitenga mnamo mwaka 2014.