1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelenskiy aishukuru Ujerumani, Ufaransa na Uingereza

Lilian Mtono
15 Mei 2023

Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine ameishukuru Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa kuipatia msaada mkubwa na muhimu wa kijeshi na kuonyesha kuridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara yake barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/4RNiC
Großbritannien | Wolodymyr Selenskyj und Rishi Sunak
Picha: Carl Court/Getty Images

Zelenskiy aidha amesema ziara hiyo imempa matumaini ya kufikiwa haraka makubaliano ya kupata ndege za kivita kutoka kwa washirika wa Magharibi. Amesema hayo baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak. 

Mapema leo Rais Volodymyr Zelenskiy alikutana na waziri mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak na kuashiria matumaini hayo ya kupata ndege za kivita, baada ya kuthibitisha kwamba walijadiliana kwa kina kuhusiana na suala hilo wakati walipokutana katika makaazi ya kupumzika ya Sunak, kaskazinimagharibi mwa London na kuyashukuru mataifa ya magharibi kwa kuendelea kuisaidia kijeshi.

"Tulizungumza kuhusu ndege za kivita, ni suala la muhimu sana kwetu kwa sababu hatuwezi kulidhibiti anga. Kwa hiyo nadhani unafahamu kila kitu kwa kina kwa sababu sisi ni washirika wa dhati. Asante sana. Na tunataka kuanzisha muungano wa ndege za kivita na ninaliunga mkono hili. Tulizungumza kuhusu hili. Na ninaona kwamba katika muda mfupi ujao tutasikia maamuzi muhimu sana," alisema Zelenskiy.

Hata hivyo amesisitiza kwamba suala hilo litahitaji kufanyiwa kazi zaidi kabla ya maafikiano.

Soma Zaidi: Zelensky kawaita Wajerumani marafiki wa kweli

Taarifa kutoka London, zilisema baada ya mazungumzo hayo kwamba Uingereza itapatia Ukraine mifumo ya kujilinda na makombora pamoja na makombora ya masafa marefu, ili kuisaidia zaidi Ukraine na kuongeza kuwa itaanza kuwapatia mafunzo ya msingi marubani wa ndege wa Ukraine katika majira haya ya joto, kama sehemu ya mkakati wake wa kushirikiana na mataifa mengine kuisadia Ukraine ndege za kivita chapa F-16. Uingereza linakuwa taifa la kwanza kutangaza hadharani kuipatia Ukraine makombora hayo.

Ukraine | Ukrainischer Panzer bei Bachmut
Picha: Libkos/AP PhotoZ/picture alliance

Katika hatua nyingine, mkuu wa Halmashauri kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen amesema hii leo kwamba mpango wa amani wa Kyiv unapaswa kutumika kama ufunguo wa juhudi zozote za kumaliza vita kati yake na Urusi, na kusisitiza kwamba ni muhimu kila mmoja kukumbuka kwamba Ukraine ilivamiwa kikatili na Urusi.

Leyen amesema hayo wakati ujumbe wa ngazi za juu wa China ukianza ziara barani Ulaya, ambayo Beijing imesema inalenga kuibua mjadala juu ya makubaliano ya kisiasa katika mzozo huo uliofikia mwezi wa 15 sasa. Leyen amesema ingawa rais wa China Xi Jinping alizungumza kwa simu na rais wa Zelensky, lakini bado kuna umuhimu wa kuutumia ushawishi wake kwa Urusi kuishinikiza kuvimaliza vita hivyo.

Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amesema anataraji hapo kesho kwamba washirika wa muungano huo watakubaliana juu ya mpango wa muda mrefu wa kuisaidia Ukraine kujiimarisha kijeshi na kufikia viwango vya NATO, katika mkutano wa kilele wa Julai, huko Vilnius.

Amesema hilo litaisaidia Ukraine kupiga hatua zaidi kusogeleea uanachama kwenye jumuiya hiyo, huku akidokeza nia yake ya kuachia ngazi mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Mjini Berlin, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema mataifa kama India, Vietnam na Afrika Kusini yanajizuia kukosoa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kwa sababu yanaamini kanuni za kimataifa hazitumiki kwa kuzingatia usawa. Amesema hayo katika hatuba yake hii leo na kuongeza kuwa mataifa hayo yanataka uwakilishi ulio sawa na si undumilakuwili kama unaoshuhudiwa sasa.