1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

WHO yatoa wito wa kupunguza mateso ya watu wa Gaza

28 Desemba 2023

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba raia wa Palestina wanakabiliwa na 'hatari kubwa' na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kupunguza mateso kwa raia wa Gaza wakati vita vikiendelea.

https://p.dw.com/p/4afbU
WHO-Chef Tedros Ghebreyesus
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza wakati wa mkutano mjini Geneva, Uswisi:07.04.2023Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

 Mashambulizi zaidi yameshuhudiwa katika mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza, eneo ambalo limekuwa kimbilio la mamia ya maelfu ya Wapalestina waliolazimika kuyahama makaazi yao upande wa kaskazini kwa maelekezo ya Israel.

Msemaji wa wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas huko Gaza, Ashraf al-Qudra, amesema watu wengine zaidi ya 200 wameuawa katika muda wa saa 24 zilizopita kufuatia mashambulizi katika eneo hilo.

Naye msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, ameeleza kuwa wametuma kikosi cha ziada cha wanajeshi huko Khan Yunis, mji alikozaliwa kiongozi wa kundi la Hamas, Yahya Sinwar.

Soma pia: Mahmoud Abbas: Israel inaendesha vita vya maangamizi Gaza

Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 80 ya jumla ya watu milioni 2.4 wa Gaza wameyahama makaazi yao, na wengi wao kwa sasa wanaishi katika makaazi duni au mahema ya muda eneo la kusini na viungani mwa mji wa Rafah unaopakana na Misri.

Nahostkonflikt - Flüchtlingsviertel Al-Maghasi
Wapalestina wakibeba mwili wa mtu aliyepatikana chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa kufuatia shambulio kubwa la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Al-Maghasi huko Deir Al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza: Desemba 25, 2023,Picha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuchukuwa "hatua za haraka ili kupunguza madhila yanayowakabili watu wa Gaza, ikiwa ni pamoja na "majeraha mabaya, njaa kali na hatari kubwa ya kukabiliwa na magonjwa".

Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi makali wakati idadi ya vifo ikiongezeka Gaza

WHO imesema katika taarifa kuwa uwezo wake wa kusambaza dawa, vifaa vya matibabu, na mafuta kwa hospitali za Gaza umekuwa ukitatizika kutokana na njaa na kukata tamaa kwa watu wanaoelekea maeneo hayo.

Israel imeapa kuiangamiza Hamas

Israel imeapa kulitokomeza kabisa kundi hilo la Hamas ambalo limeorodheshwa na Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi kadhaa za magharibi kuwa kundi la "kigaidi". Nir Barkat, Waziri wa Uchumi na Viwanda wa Israel amesema:

Israels Armeesprecher Daniel Hagari
Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagari akitoa ufafanuzi kwa vyombo vya habari kuhusu vita vya huko Gaza katika makao makuu ya Wizara ya ulinzi ya Israel mjini Tel Aviv: 18.10.2023Picha: Gil Cohen-Magen/AFP

"Tunapaswa kuweka nguvu zetu kuishughulikia Hamas na kuifuta katika uso wa dunia. Na hivyo itakuwa rahisi kujadiliana na kuwarejesha mateka wetu. Kunaweza kuwepo tofauti za maoni juu ya mambo fulani, lakini malengo yetu ya kimkakati ni sawa. Na kauli yangu kwa marafiki zetu wa Marekani ni kwamba tunaelewa jinsi ya kupigana vita hivi."

Hamas iliishambulia Israel Oktoba 7, na kusababisha vifo vya watu 1,200 wengi wao wakiwa raia, kulingana na taarifa zilizotowa na Israel ambayo imearifu pia kuwa wanajeshi wake 167 wameuawa huko Gaza.

Kwa upande mwingine,  wizara ya afya huko Gaza  inasema mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel tayari yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 21.320 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.