1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mageuzi ya Togo yanaacha nafasi ndogo ya mabadiliko

24 Aprili 2024

Siku chache kabla ya Togo kufanya uchaguzi, upinzani na mashirika ya kiraia yanasita kuamua kati ya kufanya kampeni na hofu ya ukandamizaji tangu kupitishwa kwa mageuzi ya katiba yenye utata.

https://p.dw.com/p/4f9CI
Togo Faure Gnassingbe
Rais wa Togo Faure Gnassingbe Picha: Ute Grabowsky/photothek/IMAGO

Ingawa vyama vinaendelea kufanya kampeni, matumaini ya mabadiliko ya kisiasa katika uchaguzi wa Aprili 29, ulioahirishwa mara kadhaa na serikali, ni finyu.

Jean Yaovi Degli, mwanasheria na waziri wa zamani wa uhusiano wa bunge, amesema hawapaswi kuwa na matarajio mengi katika uchaguzi ujao, akidai kwamba chama tawala hakiogopi chochote.

Togo yasogeza mbele uchaguzi wa bunge

Wabunge siku ya Ijumaa waliidhinisha mageuzi ya kubadili mfumo wa urais hadi wa bunge ambao vyama vya upinzani vinasema utamruhusu Rais Faure Gnassingbe kurefusha mamlaka yake.

Chini ya mfumo huo mpya, wabunge, badala ya wananchi, watamchagua rais ambaye atahudumu kwa miaka minne. Aidha madaraka yatahamia kwa wadhifa mpya wa rais wa baraza la mawaziri, aina ya jukumu la waziri mkuu, ambaye atakuwa kiongozi wa chama cha walio wengi katika bunge.