1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Waasi wa Houthi washambulia tena meli katika Bahari ya Shamu

10 Januari 2024

Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kwa mara nyingine tena wameshambulia meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu

https://p.dw.com/p/4b3Hy
Ndege ya waasi wa Houthi ikizunguka juu ya meli ya mizigo ya Galaxy Leader huku wapiganaji wa Houthi wakitembea juu ya meli hiyo katika bahari ya Shamu mnamo Novemba 20, 2023
Ndege ya waasi wa Houthi ikizunguka juu ya meli ya mizigo ya Galaxy LeaderPicha: Houthi Military Media/REUTERS

Kamandi kuu ya jeshi la Marekani CENTCOM imetangaza kwamba ndege za kivita za Marekani na Uingereza zimedungua droni 18 na makombora matatu ya waasi wa Houthi yaliyoelekezwa kwenye Bahari ya Shamu.

Droni zilirushwa katika njia za kimataifa za meli

Droni hizo na makombora yaliyoangushwa, yalikuwa yamerushwa kutoka maeneo ya Yemen yanayodhibitiwa na Wahouthi kuelekea Kusini mwa Bahari ya Shamu katika njia za kimataifa za meli ambapo kulikuwa na meli kadhaa za kibiashara.

Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa au uharibifu ulioripotiwa.

Soma pia:Kampuni ya meli ya Maersk kuikwepa njia ya Bahari ya Sham

Hili lilikuwa shambulio la 26 la waasi hao wa Houthi kwenye njia ya safari za meli za kibiashara katika Bahari hiyo ya Shamu tangu Novemba 19.

Mashambulizi yameongezeka tangu kuzuka kwa vita katika Ukanda wa Gaza

Tangu kuzuka kwa vita vya Gaza kati ya Israeli na kundi la wanamgambo wa Hamas, waasi wa Houthi wameshambulia mara kwa mara meli hizo za kibiashara kwa madai ya kuhusika kwa Israel katika Bahari ya Shamu.

Soma pia:Marekani yazima shambulizi ya Wahouthi huko Bahari ya Shamu

Jeshi la Marekani liliimarisha ushirikiano wake na vikosi vya kijeshi vya nchi nyingine katika eneo hilo katikati ya mwezi Desemba.

Picha iliyochukuliwa wakati wa ziara iliyopangwa ya waasi wa Houthi mnamo Novemba 22, 2023, inayoonesha meli ya Galaxy Fighter iliyotekwa na waasi hao siku mbili kabla
Meli ya Galaxy Fighter iliyotekwa na waasi wa HouthiPicha: Houthi Media Centre/AFP

Waasi hao wa Houthi wamesema wataruhusu tu meli zinazopeleka msaada katika Ukanda wa Gaza kupitia eneo hilo la bahari.

Meli kadhaa zimeshambuliwa tangu wakati huo ikiwa ni pamoja na meli ya mizigo ya kampuni ya Ujerumani ya Hapag-Lloyd.

Kampuni kubwa za usafirishaji wa meli zinazidi kukwepa njia ya kupita Bahari ya Shamu.

Rasimu ya azimio la Marekani itakayopigiwa kura

Rasimu ya azimio la Marekani, iliyoonekana Jumanne jioni na shirika la habari la AP, imesema kuwa takriban mashambulizi 12 ya waasi wa Houthiyanazuia biashara ya kimataifa pamoja na kudhoofisha haki za usafiri na uhuru pamoja na amani na usalama wa kikanda.

Yaliomo katika azimio la Marekani

Azimio hilo linataka  kuachiliwa mara moja kwa meli ya kwanza iliyoshambuliwa na waasi hao wa Houthiya Galaxy Leader, inayoendeshwa na Japan na yenye uhusiano na kampuni ya Israeli ambayo waasi hao waliiteka mnamo Novemba 19 pamoja na wafanyakazi wake.

Marekani na nchi nyingine zatishia hatua za pamoja

Wiki iliyopita Marekani na nchi nyingine 12 zilitoa taarifa ya wito wa kusitishwa mara moja kwa mashambulizi hayo ya wa Houthi na kuonya kwamba mashambulizi zaidi yatahitaji hatua za pamoja.

Soma pia:Marekani yazindua muungano wa ulinzi wa Bahari ya Shamu kulinda meli dhidi ya mashambulizi ya waasi wa Houthi

Mataifa hayo yalisema kuwa waasi hao wa Houthi watakabiliwa na athari za vitendo hivyo iwapo wataendelea kutishia maisha, uchumi wa dunia, na mtiririko huru wa biashara  katika njia kuu za bahari katika kanda hiyo.