1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi wasema uchaguzi wa Togo ulikuwa huru

Hawa Bihoga
30 Aprili 2024

Waangalizi wa uchaguzi Jumuiya ya Mataifa ya Sahel (CEN-SAD) wamesema uchaguzi wa wabunge nchini Togo unapaswa kuchukuliwa kuwa "huru, haki na wazi", siku moja baada ya taifa hilo la Afrika Magharibi kuchaguwa wabunge.

https://p.dw.com/p/4fMlV
Rais Faure Gnassingbé wa Togo.
Rais Faure Gnassingbé wa Togo.Picha: Filip Singer/EPA Pool/dpa/picture alliance

Jumuiya hiyo ya CEN-SAD ilisema kwenye taarifa yake kwamba uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira mazuri na bila matukio yoyote makubwa. 

Hadi wakati jumuiya ya CEN-SAD ilipokuwa inatoa kauli yake, Tume ya Uchaguzi ya Togo ilikuwa humo haijatoa hata matokeo ya awali, kufuatia uchaguzi huo wa bunge uliofanyika baada ya wabunge kupitisha mageuzi ya katiba yanayopingwa na makundi ya upinzani yakisema yatamuongezea muda wa kukaa madarakani Rais Faure Gnassingbe.

Soma zaidi: Togo yapiga kura ya wabunge baada ya mageuzi ya kikatiba

Chama kikuu cha upinzani nchini Togo, National Alliance for Change, nacho hakikuwa kimetoa tamko lolote kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo, lakini muungano wa upinzani (DMP), ulisema uliona hitilafu katika vituo kadhaa, ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa kuanza kwa upigaji kura.

Tayari Gnassingbe ameshinda chaguzi nne tangu 2005, zote zikikosolewawa na upinzani.