1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin: Urusi haitaruhusu vitisho

Angela Mdungu
9 Mei 2024

Rais wa Urusi Vladimir ameyatuhumu mataifa ya magharibi kwa kutaka kuitumbukiza dunia katika mgogoro na kuongeza kuwa hakuna atakayeruhusiwa kulitishia taifa lenye uwezo mkubwa wa nyuklia.

https://p.dw.com/p/4fg5I
Gwaride la jeshi la Urusi
Gwaride la jeshi kuadhimisha Siku ya Ushindi UrusiPicha: Vladimir Smirnov/TASS/dpa/picture alliance

Ameyasema hayo wakati leo Urusi ikiadhimisha miaka 79 ya ushindi wa umoja wa Kisovieti dhidi ya utawala wa Kinazi wa Ujerumani katika vita vya pili vya dunia.

Maadhimisho hayo ya 'Siku ya Ushindi ' yameongozwa  na rais Vlamdir Putin mapema Alhamisi mjini Moscow. Katika tukio hilo wanajeshi 9,000 wameshiriki katika gwaride la heshima ambapo 1,000 kati yao walikuwa sehemu ya waliopigana katika vita nchini Ukraine, tangu Urusi ilipolivamia taifa hilo mwaka 2022.   Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho hayo, Rais Putin ametoa tahadhari kuwa, Urusi itafanya kila kitu kuzuia mzozo wa kimataifa, lakini haitaruhusu mtu yeyote aitishe. Amesema Vikosi vyake vya kimkakati viko makini wakati wote".

Putin ambaye ameanza muhula wake wa tano madarakani ameongeza kuwa siku hii ya ushindi kwa Urusi ambayo ni ya mapumziko kote Urusi, inaviunganisha vizazi vyote. Ameongeza kuwa taifa hilo linasonga mbele kwa kutegemea tamaduni zake huku watu wa taifa hilo wakiwa na uhakika wa kuhakikisha uhuru  wa Urusi na mustakabali salama.

Putin amdai ataifa ya magharibi yanachochea mizozo ya kikanda

Ameitumia sehemu ya hotuba yake kuwapongeza wanajeshi wake kwa mapambano dhidi ya Ukraine na kudai kuwa mataifa ya magharibi yanachochea mizozo ya kikanda, kikabila na ya kidini. Rais huyo wa Urusi ametoa karipio kali kwa mataifa hayo huku akizikumbusha nchi hizo juu ya uwezo wa Urusi wa nyuklia.

Urusi yaadhimisha siku ya ushindi
Rais wa Urusi Vladmir PutinPicha: Alexei Druzhinin/dpa/Sputnik Kremlin/AP/picture alliance

Zaidi Putin amewaambia watu waliohudhuria kumbukumbu hiyo kuwa, Urusi inapitia wakati mgumu, na kuwa hatma ya taifa hilo inamtegemea kila mmoja wao. Shamrashamra za maadhimisho hayo zimehudhuriwa  na viongozi nane wa yaliyokuwa mataifa ya Umoja wa Kisovieti ambayo ni Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan. Viongozi wa  Laos na Guinea-Bissau pia walikuwemo.

Soma zaidi: Siku ya ushindi Putin awapongeza wanajeshi wake kwa kuitetea nchi yao

Itakumbukwa kuwa, vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya wanajeshi wa Ujerumani kuipoingia Poland mwezi Septemba 1939. Vilimalizika mara mkuu wa majeshi wa Ujerumani, Wilhelm Keitel, aliposaini waraka wa kujisalimisha usiku wa manane Mei 8, kwenye makao makuu ya jeshi la Kisovieti mjini Berlin. Katika vita hivyo, watu takriban milioni 70 waliuwawa kote duniani, milioni 27 kati yao walikuwa kutoka Muungano wa Usovieti.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Vladmir Putin ameyafanya maadhimisho ya kumalizika kwa vita hivyo kuwa sehemu muhimu ya ajenda yake ya kisiasa huku akionesha uwezo wa kijeshi wa taifa lake.