1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vizuizi vya Israel ukanda wa Gaza vimeathiri uchumi

26 Novemba 2020

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatano inasema vizuizi vilivyowekwa na Israel katika ukanda wa Gaza unaotawaliwa na kundi la Hamas, vimeathiri uchumi, kusababisha umaskini mkubwa na ukosefu wa ajira.

https://p.dw.com/p/3lqBQ
Palästina Auschreitungen im Gazastreifen
Picha: picture alliance / ZUMAPRESS.com

Israel ilianzisha vizuizi hivyo mwaka 2007, baada ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas linalopinga uwepo wa Israel, kulidhibiti eneo la Gaza kutoka mikononi mwa vikosi vya mamlaka inayotambulika kimataifa ya Palestina. Hatua za Israel sambamba na vizuizi vya nchi jirani ya Misri, zimezuia harakati za watu na bidhaa ndani na nje ya eneo hilo. Israel inadai kuwa vizuizi hivyo vinahitajika ili kulizuia kundi la Hamas kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.

Ripoti hiyo ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu  biashara na maendeleo, imeunga mkono wito wa mashirika mbalimbali ya kimataifa wa kukosoa vizuizi vya Israel, ambavyo wanasema ni adhabu na vinaumiza maisha ya wakaazi wapatao milioni mbili ndani ya Gaza, huku vikishindwa kuliondoa kundi la Hamas katika eneo hilo.

Gaza kwa kiwango kikubwa inakabiliwa na ukosefu wa maji safi ya kunywa, kukatika mara kwa mara kwa umeme na raia wake kukosa uhuru wa kusafiri nje ya nchi. "Matokeo yake ni karibu kuanguka kwa uchumi wa mkoa wa Gaza na kutengwa kwake na uchumi wa Wapalestina na maeneo mengine ya ulimwengu", imesema taarifa ya Umoja wa Mataifa.

Palästina Blockade Gazastreifen Grenze zu Israel Grenzzaun
Tumekwama hapa sijui kama tutafunguliwaPicha: Imago/UPI Photo

Ripoti hiyo ilichambua athari zote za vizuizi ambazo zimepunguza uwezo wa Gaza wa kusafirisha bidhaa pamoja na athari za vita vya mara tatu ambavyo vilitokea kati ya mwaka 2008-2009, 2012, na 2014. Vita vya mwisho ndivyo vilikuwa vibaya zaidi na kuwaua Wapalestina zaidi ya 2000, nusu wakiwa ni raia na wengine 100,000 kukosa makaazi kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa umesema Gaza imeshuhudia moja ya hali mbaya ya kiuchumi ulimwenguni, ikiongeza kuwa kunahitajika hali ya haraka ya kuondoa vizuizi ili watu wake waweze kufanya biashara kwa uhuru na maeneo mengine yanayokaliwa na Wapalestina na ulimwengu kwa ujumla.

Msemaji wa Hamas Hazem Qassem amesema ripoti hiyo ina dhihirisha "uhalifu unaofanywa na Israel. "Kuzingirwa huku kumesababisha uhalifu wa kivita na kuchangia sekta zote za huduma kuanguka katika ukanda wa Gaza" alisema. "Takwimu hizi pia zinaonyesha kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kushughulikia kuzingirwa kinyume cha sheria kwa Gaza. "

Israel iliyatwaa maeneo ya ukingo wa Magharibi, Jerusalem mashariki na ukanda wa Gaza katika vita vya mashariki ya kati mwaka 1967, ingawa ilijiondoa Gaza mwaka 2005. Ripoti hiyo imeorodhesha mapendekezo kadhaa kuisaidia Gaza kuelekea njia ya maendeleo endelevu, ingawa imesema kwa upande mwingine kuwa mahsambulizi ya maroketi dhidi ya raia wa Israel ni kinyume chini ya sheria za kimataifa.