1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUswisi

Vita vya Ukraine vyagubika kongamano la kiuchumi la Davos

Sylvia Mwehozi
17 Januari 2023

Vita vya Ukraine na vitisho vya mdororo wa uchumi ulimwenguni ni mada zinazotawala Kongamano la kila mwaka la uchumi duniani, WEF, ambalo limeanza leo katika mji wa Davos nchini Uswisi.

https://p.dw.com/p/4MINw
Schweiz I WEF in Davos
Picha: Laurent Gillieron/KEYSTONE/picture alliance

Ndege za kijeshi, wanajeshi na polisi wamesambazwa katika mji huo wa kifahari wakati viongozi wa serikali, wakurugenzi, wanaharakati na watu mashuhuri wakikusanyika kwa kongamano hilo la kiuchumi la kila mwaka. Kongamano hilo limerejea tena katika utamaduni wake wa kufanyika wakati wa msimu wa baridi baada ya miaka mitatu ya kutatizwa na janga la Covid-19, hali iliyolazimu mkutano huo kufanyika kwa njia ya mtandao.Ni yapi yaliyojitokeza Davos?

Kongamano hilo litakalofanyika kwa wiki nzima limeanza chini ya kauli mbiu ya "ushirikiano katika ulimwengu uliogawanyika" wakati sayari inakabiliwa na dhoruba kubwa ya migogoro, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mfumuko wa bei unaozidi kuongezeka, hali ya mdororo wa uchumi na majanga ya mazingira".

Mwasisi wa jukwaa hilo la kiuchumi WEF ambaye ni mwanauchumi wa Ujerumani Klaus Schwab alisema kwamba kongamano la mwaka huu linafanyika katika nyakati ngumu wakati ulimwengu ukikabiliwa na "mizozo mingi kwa wakati mmoja."

WWF Davos 2023 Auftakt/Protest
Wanaharakati wa mazingira wakiandamana kando ya komgamano la DavosPicha: Arnd Wiegmann/REUTERS

Mzozo wa Ukraine ambao umeilazimu Urusi nje ya mkutano huo wa Davos, kwa mara nyingine utagubika mazungumzo hayo. Viongozi wa nchi za Ulaya akiwemo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg watatoa hotuba zao kesho Jumatano.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatazamiwa kuhutubia kwa njia ya video leo Jumanne huku mawaziri wa Ukraine, viongozi wa kijeshi, mameya na wanajeshi wanaunda mojawapo ya jopo kubwa la ujumbe wa Kyiv watakapojaribu  kuomba silaha zaidi na msaada wa kifedha kutoka nchi za Magharibi. Soma: Mamia waandamana Davos kupinga uroho wa mataifa tajiri

Nchi tajiri kiuchumi zatakiwa kupunguza umasikini duniani

China pia inatuma ujumbe wa ngazi ya juu wakati ikirejea tena baada ya kuondoa vizuizi wiki iliyopita kufuatia miaka mitatu ya vizuizi vikali vya kupambana na Covid-19. Mzozo wa gharama za maisha sambamba na ule wa nishati pamoja na usambazaji wa chakula, ndio vitisho vya muda mfupi duniani, kulingana na ripoti ya kila mwaka ya jukwaa la WEF wakati wachumi wengi wakitabiri kuporomoka kwa uchumi duniani kwa mwaka huu wa 2023. Mwigizaji mashuhuri Idris Elba ambaye ni balozi wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD yuko mjini Davos, kuwahimiza viongozi wa kisiasa na wakurugenzi kuwasaidia wakulima wadogo barani afrika.

"Nadhani sasa kinachonisukuma ni kukosekana usawa wa nusu ya ulimwengu kula chakula na nusu ya ulimwengu kutokula. Na nusu ya dunia inasababisha uharibifu mkubwa kwa sayari na nusu nyingine haichangii lakini inateseka na njaa kutokana na uharibifu huo. Hiyo ni dhuluma. Ingekuwa sinema, hao ndio watu wabaya na hawa ndio wazuri."

Mabadiliko ya tabia nchi pia yatakuwa moja ya mada kuu, huku mjumbe wa mazingira wa wa Marekani John Kerry akiwa miongoni mwa wazungumzaji. Waandaaji wana shauku ya majadiliano ili kusaidia maandalizi ya duru ijayo ya mazungumzo ya mazingira duniani, COP28, ambayo yatafanyika katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu iliyo mzalishaji wa mafuta kuanzia Novemba 30.