1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU wakutana kujadili mfuko wa ufufuaji uchumi

Sekione Kitojo
17 Julai 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana  leo Ijumaa (17.07.2020) katika ukumbi mkubwa katika mkutano wao wa kilele ili kuweza kukaa mbali mbali kama tahadhari ya kiafya kutokana na ugonjwa wa COVID-19 licha ya tofauti zao.

https://p.dw.com/p/3fTWh
Belgien Brüssel EU-Gipfel | Sitzungssaal
Picha: Reuters/F. Lenoir

Lakini  hiyo sio hali pekee  ambayo  viongozi  hao  wanajikutana wakiwa mbali kutoka  kila  mmoja katika  mkutano kama  huo, lakini mpango wa  bajeti  ya  Umoja  wa  Ulaya  ya Trilioni 1.85 na  mfuko wa  ufufuaji  uchumi unawaweka  mbali mbali  kimtazamo. 

Belgien  EU Ratsitzung  Treffen EU Rat Brüssel
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiwa tayari mjini Brussels tayari kwa mkutano wao muhimuPicha: Reuters/S. Lecocq

Rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron  aliongoza  majadiliano  ya mapema, akiwasili jana na  kutumia  saa  za  mwanzo  kabla  ya mkutano  kukutana  na  waziri  mkuu  wa  Uholanzi  Mark Rutte, mtu mwenye msimamo  mkali  kabisa  kuhusu  kubana  matumizi ya  bajeti na  anayeonekana  kuwa  mmoja  kati ya  kikwazo  kikubwa  katika kufikiwa  makubaliano  katika  mkutano huo  wa  siku  mbili.

Mkutano  huo  unaweza  kuchukua  muda  mrefu  zaidi, kama itakuwa  muhimu, kuondoa  tofauti zilizopo  baina  ya  viongozi.

Changamoto  zinazoyakabili  mataifa  27  ya  Umoja  wa  Ulaya  ni kubwa. Kundi  hilo  la  mataifa  linasumbuka kutokana  na  mdororo mbaya  zaidi  katika  historia  na  mataifa  wanachama yanapambana  juu  ya  nani  atalipa zaidi  kusaidia  mataifa  mengine na  mataifa  gani  yanapaswa  kupata  fedha  zaidi  ili  kubadili mwelekeo wa  uchumi  wao  ulioathirika.

EU Gipfel Merkel und von der Leyen (farblich) in Einklang mit Wilmes und Marin
Waziri mkuu wa Ubelgiji Sophie Wilmes, rais wa halmashari ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Finland Sanna Marin wakiwa tayari kwa mkutano huo mjini Brussels.Picha: Reuters/S. Lecocq

Mzozo  uliosababishwa  na  janga  la  virusi  vya  corona,  pamoja na  madhara  yake  yote  ya  kiuchumi  na  kijamii, ni mbaya  sana ambao  hatujawahi  kukumbana  nao  tangu  vita  vikuu  vya  pili  vya dunia," rais  wa  baraza  la  Ulaya  na mwenyekiti  wa  mkutano  huo Charles Michel  amesema  jana  jioni.

Matumaini kwa Merkel 

Wajumbe  watapunguzwa  kufikia  tu idadi ya  wastani, wakiachwa  viongozi wakitegemea  tu  ujuzi wao  binafsi  katika  maelezo ya  waraka  huo tata. Tangu  kuzuka  kwa  janga  la  virusi vya  corona kansela wa Ujerumani  Angela  Merkel , anaonekana  kuwa ana uwezo wa kuiongoza  nchi  yake kupita katika  mzozo huu na  hivi  sasa  ikiwa Ujerumani  inashikilia  urais wa  kupokezana  wa  Umoja  wa  Ulaya,  nafasi  yake itakuwa  kubwa  zaidi  katika  mkutano  huu. Alipowasili jana  mjini  Brussels  alisema.

"Tunakutana leo kwa  mara  ya  kwanza  kuhuu suala  la  mfuko wa kufufua  uchumi utakaotuwezesha  kuwa  imara  kwa  siku  zijazo. Majadiliano  yetu mwezi Februari  hayakufikia  mafanikio. Tumefanya matayarisho mengi lakini sasa  tunajikuta  katika  hali  tofauti  na ilivyokuwa mwezi Februari. Na  ndio sababu  tunaingia  katika majadiliano  haya  kwa  matumaini makubwa , pamoja  na  kwamba tofauti zetu  ni  kubwa , lakini  mara  hii tutapata matokeo."

Belgien Brüssel EU-Gipfel | Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture-alliance/AP Images/J. Thys

Mataifa  wanachama  walikuwa  wakipambana  vikali  kuhusu  bajeti ya  miaka saba ya  Umoja  wa  Ulaya  ya  trilioni 1.85 wakati COVID-19 ilikuwa ni taarifa ndogo  tu  kutoka  Wuhan, China mwishoni  mwa mwaka  jana. Baada  ya  hapo  virusi  hivyo  vilishambulia  mataifa ya  Umoja  wa  Ulaya  kwa  nguvu  zote  na  makadirio  hivi  sasa  ni kwamba  uchumi wa  mataifa  19 yanayotumia  sarafu ya  euro utanywea kwa  asilimia 8.7 mwaka  huu.