1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yakubali kuiunga mkono Sweden kujiunga NATO

11 Julai 2023

Uturuki imekubali kuliunga mkono ombi la Sweden kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na itawasilisha uamuzi huo haraka iwezekanavyo ili uidhinishwe na bunge lake mjini Ankara.

https://p.dw.com/p/4TiJr
Natogipfel in Litauen Eingung zwischen Erdogan und Ulf Kristersson
Picha: Henrik Montgomery/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, ambaye alikutana kwa mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Waziri Mkuu Ulf Kristersson wa Sweden mjini Vilnius, Lithuania, kunakoanza mkutano wa kilele wa siku mbili wa NATO.

Soma zaidi: Erdogan aondoa pingamizi kwa Sweden kujiunga na NATO
Mkutano wa NATO kuanza Jumanne nchini Lithuania

Hata hivyo, taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao watatu haijabainisha ni kwa muda gani bunge la Uturuki litalazimika kuidhinisha ombi hilo la Sweden.

"Kukamilisha ombi la Sweden ni hatua ya kihistoria inayonufaisha usalama wa washirika wote wa NATO hasa katika wakati huu muhimu," alisema Stoltenberg.