1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripota wa gazeti la Wall Street azuiliwa Urusi

Bruce Amani
30 Machi 2023

Mahakama moja mjini Moscow imeamuru kuwa mwandishi habari wa Kimarekani wa jarida la Wall Street anapaswa kuzuiliwa kwa karibu miezi miwili kwa tuhuma za kuifanyia Washington upelelezi.

https://p.dw.com/p/4PWBI
USA Evan Gershkovich Journalist
Picha: AFP/Getty Images


Hiyo ndio hatua kali kabisa kuwahi kufanywa dhidi ya mwandishi habari wa kigeni tangu Urusi ilipoivamia Ukraine. Idara ya ujasusi ya Urusi - FSB imesema mapema leo kuwa imeanzisha kesi ya jinai dhidi ya raia wa Marekani Evan Gershkovich kwa tuhuma za upelelezi na Kremlin imesema alinaswa wakati akifanya kitendo hicho.

Gershkovich ambaye amekuwa akilifanyia kazi gazeti hilo kwa mwaka mmoja tu, ameiambia mahakama kuwa hana hatia. Mwajiri wake amesema kesi dhidi yake inatokana na madai ya uwongo.

Upelelezi chini ya sheria ya Urusi una adhabu ya hadi miaka 20 jela. Kesi hiyo itaharibu hata zaidi mahusiano ambayo tayari ni mabaya kati ya Urusi na Marekani ambayo ndiyo nchi kubwa kabisa inayoiunga mkono kijeshi Ukraine na imeiwekea Moscow vikwazo ili kujaribu kuishawishi kuwaondoa askari wake.