1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kutoa ripoti ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Bruce Amani
20 Machi 2023

Umoja wa Mataifa unaratajiwa kutoa ripoti inayotoa tathmini ya kisayansi ya karibu muongo mmoja kuhusu athari na mwenendo wa ongezeko la joto duniani na mbinu zilizopo za kuzuia maafa ya tabianhchi

https://p.dw.com/p/4Ov5y
Kenia Dürre an der Grenze zu Äthiopien
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Ripoti hiyo iliyotengenezwa na mamia ya wanasayansi wakuu ulimwenguni ilitakiwa kuidhinishwa na wajumbe 650 wa serikali mbalimbali Ijumaa iliyopita mwishoni mwa mkutano wa wiki nzima katika mji wa Uswisi wa Interlaken.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa mwito kwa wajumbe mwanzoni mwa mkutano huo kutoa kile alichokiita ukweli mtupu na mchungu ili kuwasilisha ujumbe kuwa muda unayoyoma kwa ulimwengu kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzijoto 1.5 za celcius ikilinganishwa na nyakati za kabla ya mapinduzi ya kiviwanda. "Ulimwengu upo katika njiapanda na sayari yetu ipo kwenye shabaha. Tunakaribia hatua ya kutorudi nyuma, ya kuvuka kikomo kilichokubaliwa kimataifa cha nyuzijoto 1.5 za celcius cha ongezeko la joto duniani. Ripoti zenu za karibuni pia zimesisitiza haja ya kuchukua hatua sasa."

Frankfurt | Fridays For Future Proteste
Maandamano ya kudai hatua dhidi ya ongezeko la jotoPicha: Michael Probst/AP/picture alliance

Makubaliano hayo yaliahirishwa mara kadhaa huku maafisa kutoka mataifa makubwa kama vile China, Brazil, Saudi Arabia, Marekani na Umoja wa UIaya yakijadiliana mwishoni mwa juma kuhusiana na maneno ya vifungu muhimu vya rasimu hiyo.

Soma piaCOP15 wafikia mafikiano kihistoria kuhusu bioanuwai

Ripoti hiyo ya Jopo la Kiserikali la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi – IPCC inajumuisha msururu wa utafiti kuhusu ongezeko la joto ulimwenguni uliofanywa tangu kufikiwa muafaka wa Paris wa tabianchi mnamo mwaka wa 2015.

Mukhtasari wa ripoti hiyo uliidhinishwa mapema jana lakini makubaliano ya chapisho kuu yaliendelea kwa masaa kadhaa zaidi, huku baadhi ya waangalizi wakihofia kuwa huenda litahitaji kuahirishwa. Umoja wa Mataifa unapanga kuichapisha ripoti hiyo mchana huu.

Mchakato usio wa kawaida wa kuzitaka nchi kuidhinisha ripoti ya kisayansi unanuia kuhakikisha kuwa serikali zinakubali matokeo yake kama ushauri wenye mamlaka ambao hatua zao zitauzingatia.

Mabadiliko ya Tabianchi yatibua ladha ya Mbege

Waangalizi wanasema mikutano ya IPCC imeendelea kuingizwa siasa huku maslahi ya kupunguza ongezeko la joto duniani, yakiakisi mazungumzo ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa ya tabianchi ambayo kawaida hufanyika mwishoni mwa mwaka.

Miongoni mwa masuala tete kabisa katika mkutano wa karibuni ni jinsi ya kufafanua ni mataifa gani yanayohesabika kuwa nchi zinazoendelea zilizo hatarini, na kuzifanya kustahiki kupata fedha kutoka kwa kile kinachofahamika kama mfuko wa "hasara na uharibifu” uliokubaliwa katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ya tabianchi nchini Misri.

Wajumbe pia wamepambana kuhusu tarakimu wakieleza kiasi gani uzalishaji wa hewa chafu unahitaji kupunguzwa katika miaka ijayo, ma jinsi ya kujumuisha juhudi za kibinaadamu au za kiasili za kupunguza gesi ya kaboni.

Kama nchi ambayo imetoa kiwango kikubwa zaidi cha hewa ya ukaa katika angahewa tangu kuanzishwa kwa viwanda, Marekani inaipinga vikali dhana ya wajibu wa kihistoria wa mabadiliko ya tabianchi

afp, dpa, ap