1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Hali katika hospitali za Gaza ni mbaya mno

18 Januari 2024

Umoja wa Mataifa umesema Wapalestina wanaendelea kufa kila siku huko Gaza huku hospitali zilizosalia zikiwa zimediwa na haziwezi kutoa huduma kwa makumi ya maelfu ya watu waliojeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4bQhY
Vita vya Gaza- Hospitali ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza
Raia wa Palestina waliojeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel wakipatiwa matibabu kwenye hospitali ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza: 03.11.2023Picha: Saeed Jaras/APA/IMAGO

Mtaalam wa masuala ya dharura wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Sean Casey amesema hospitali zilizosalia za Gaza haziwezi kukabiliana na idadi ya watu waliojeruhiwa, ambapo Wizara ya Afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas ikikadiria kuwa zaidi ya watu 60,000 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa vita hivyo huku mamia ya wengine wakijeruhiwa kila siku.

Casey ambaye pia ni mratibu wa kikosi cha Matibabu ya Dharura anasema madaktari na wauguzi watano au sita wanawashughulikia mamia ya wagonjwa kwa siku na kwamba alishuhudia wagonjwa wengi waliolala sakafuni na huwezi kutembea katika hospitali hizo bila kukanyaga mikono au miguu ya wagonjwa hao."

Aidha Casey, ambaye hivi majuzi alifanya ziara ya wiki tano katika eneo hilo la Palestina lililokumbwa na vita amesema:

Vita vya Gaza- Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza
Wagonjwa na raia wa Palestina wakiwa katika hospitali ya Al-Shifa huko Gaza: 10.11.2023Picha: Khader Al Zanoun/AFP

" Nimeshuhudia mara kadhaa maafa ya kibinadamu yanayotokea. Tunayashuhudia kila siku huko Gaza, na hali ikizidi kuwa mbaya zaidi, huku tukishuhudia kusambaratika kwa mfumo wa afya siku baada ya siku. Hospitali zinafungwa, wahudumu wa afya wanakimbia huku majeruhi wakiendelea kumiminika. Kunashuhudiwa pia ukosefu wa dawa na vifaa vya matibabu pamoja na ukosefu wa mafuta kwa ajili ya jenereta za hospitali zinazowezesha kupata umeme na mashine kufanya kazi."

Soma pia: WHO yaitaja hospitali ya Al Shifa kama "eneo la kifo"

Mtaalam huyo wa WHO amesema Hospitali kubwa zaidi ya Gaza ya Al-Shifa ambayo ilikuwa na jumla ya vitanda 700, kwa sasa hutoa matibabu kwa majeruhi na wagonjwa wenye uhitaji wa dharura. Hospitali hiyo imekuwa pia kimbilio la maelfu ya watu ambao wanaishi katika vyumba vya upasuaji na sehemu zengine.

Hali mbaya ambayo haijawahi kushuhudiwa

Daktari wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu (ICRC) ameielezea hali katika hospitali za Gaza kuwa mbaya zaidi na ambayo haijawahi kushuhudiwa.  Kulingana na WHO ni hospitali 15 pekee kati ya 36 ndizo zinazofanya kazi huko Gaza.

Rais wa Israel Isaac Herzog
Rais wa Israel Isaac Herzog akiwa katika makazi yake mjini Beit HaNassi huko Jerusalem: 24.10.2023Picha: Nicolas Messyasz/abaca/picture alliance

Hayo yakiarifiwa , Rais wa Israel Isaac Herzog akizungumza katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos amesema Israel "inaomba" shehena ya dharura ya dawa inayotumwa kwenye mpaka wa Gaza kupitia Misri itawafikia mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas.

Soma pia: WHO yalaani shambulio la Israel dhidi ya hospitali Gaza

Wakati huo huo nchi ya Jordan imesema Israel inapaswa kuwaruhusu Wapalestina waliokimbia makazi yao huko Gaza kurejea makwao. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan mjini Amman. Kulingana na Safadi, ni muhimu kukomesha vita huko Gaza na kuepusha kuongezeka kwa ghasia katika eneo hilo.

(Vyanzo: Mashirika)