1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na India kushirikiana kulinda mazingira

Lilian Mtono
6 Desemba 2022

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema taifa hilo linalenga kushirikiana na India katika kuimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/4KYdV
Außenministerin Baerbock besucht Indien
Picha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Waziri Annalena Baerbock amesema hayo katika siku ya pili ya ziara yake rasmi nchini India ambapo pia amesifu juhudi za India za kujiimarisha katika matumizi ya nishati mbadala na kuachana na mafuta ya visukuku. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Ujerumani amesema mzozo wa kimazingira umekuwa kitisho kikubwa kwa muongo sasa kwa kila mmoja ulimwenguni, alipokuwa akizungumza kwenye kongamano huko New Delhi kuhusiana na vipaumbele vya Ujerumani kuelekea ukanda wa Bahari ya Hindi na Pasifiki.

Amesisitiza kwamba hakuna jeshi litakaloweza kuwalinda dhidi ya mzozo wa mazingira na kwa maana hiyo wanalazimika kushirikiana kukabiliana na kitisho hicho.

Alhamisi iliyopita, India ilichukua uenyekiti wa kundi la G20 ambalo kwa kiasi kikubwa linakutanisha mataifa yaliyoendelea kiuchumi, na kauli mbiu ya kiti hicho ni "Dunia Moja, Familia Moja, Mustakabali mmoja". Baerbock amesema kauli mbiu hiyo ya India inaakisi umuhimu wa kusimama pamoja kama familia ili kusonga mbele. 

Außenministerin Baerbock besucht Indien
Waziri Baerbock alitembelea na kushuhudia mifumo ya umwagiliaji inayotumia nishati ya jua akiwa nchini India.Picha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

India likiwa ni taifa la pili kwa idadi kubwa ya watu ulimwenguni, ikitanguliwa na China inashika nafasi ya nne katika uzalishaji wa hewa ya ukaa. Utegemezi wake kwenye nishati mbadala na makaa ya mawe kwa sasa unazidi kuongezeka, wakati ikiangazia kuachana na nishati zinazozalisha kaboni ifikapo mwaka 2070.

Soma Zaidi:Idadi ya watu kufikia bil.8 ifikapo Novemba

Baerbock ashuhudia miradi ya nishati mbadala ili kulinda mazingira.

Kwenye ziara hiyo rasmi na ya kwanza nchini India, Baerbock ametembelea pia kijiji cha Khori, kilichopo nje ya jiji la New Delhi na kukutana na wakuu wa shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na masuala ya mikopo midogomidogo, nishati jadidifu, upandaji miti na uwezeshaji wa wanawake kwenye jamii.

Akiwa kwenye kijiji hicho, Baerbock amesifu juhudi za India za kuimarisha matumizi ya nishati mbadala na kujizuia kutumia mafuta ya visukuku kama namna moja wapo ya kuondokana na umasikini.

Baerbock aidha alishuhudia mifumo ya nishati ya jua ambayo imekuwa ikitumika kusambaza umeme kwenye makazi ya watu pamoja na mabomba yanayotumia umeme huo wa jua kumwagilia mashamba ya haradali, wakati taifa hilo likiendeleza ujenzi wa mifumo mikubwa ya nishati ya jua kwa ajili ya umwagiliaji.

Ziara yake ya siku mbili imekamilika hii leo na kwa kiasi kikubwa imeashiria namna ambavyo Ujerumani inaangazia kushirikiana kwa karibu na India.

Mashirika: DPAE