1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Marekani na Israel kwenye mtihani mzito

Tatu Karema
5 Aprili 2024

Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa na sera moja ambayo vyama vya Democratic na Republican vinakubaliana nayo: uhusiano thabiti kati ya Marekani na Israel usiobadilika kwa namna yoyote ile, lakini hilo sasa linaingia doa.

https://p.dw.com/p/4eTpz
Benjamin Netanjahu na Joe Biden
Benjamin Netanjahu na Joe Biden.Picha: Michael Gottschalk/picture alliance/photothek

Viongozi wa vyama vyote hivyo viwili wameshikilia misimamo kuwa Israel haina mshirika wa karibu zaidi ya Marekani na kwamba usalama wa nchi hiyo sio suala la mjadala.

Kwa mujibu wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni, tangu mwaka 1948, Israel imepokea takriban dola bilioni 280 za msaada kutoka Marekani, kiasi kikubwa kikiwa msaada wa kijeshi.

Kiwango hicho ni takribani mara mbili ya msaada ipatiwayo Misri, taifa la pili la kwa upokeaji msaada mkubwa wa Marekani lakini lenye idadi ya watu milioni 111 ikilinganishwa na Israel yenye idadi ya watu milioni 9.5 tu.

Soma zaidi: Baraza la Haki la UN lataka Israel kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita huko Gaza

Chuck Freilich, naibu mshauri wa zamani wa usalama wa kitaifa wa Israel, ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika vyuo vikuu vya Columbia, New York na Tel Aviv, aliiambia DW kwamba uhusiano kati ya mataifa hayo hauna mfano.

"Maadili ya pamoja, maslahi ya kimkakati na ushawishi mkubwa unaoiwekaIsraelkatika vitabu vizuri vya Marekani, ndizo nguzo kuu za uhusiano huo." Anasema Freilich.

Baada ya Marekani kukabiliwa na ukosoaji wa kutochukuwa hatua za kutosha kuwaokoa Wayahudi barani Ulaya kutokana na mauaji ya wakati wa enzi ya Wanazi, ilikuwa rahisi kulitambua taifa la Israel wakati viongozi wa harakati za Kizayuni walipotangaza uhuru wao mnamo Mei 1948.

Maandamano ya kupinga Israel New York
Maandamano ya kupinga vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika jijini New York tarehe 28 Machi 2024.Picha: Andrew Kelly/REUTERS

Tangu wakati huo, Israel imejitangaza kama demokrasia huru inayozingatia maslahi ya Marekani katika eneo ambalo mara nyingi si rafiki kwa taifa hilo.

Mambo yalipogeuka

Mashambulizi ya Israel ya zaidi ya miezi sita katika Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 33,000 na kuchochea shutuma za kimataifa.

Sasa, utawala wa Biden unazungumzia kuhusu kutoichanganya serikali ya Israel na watu wa Israel kama vile Makamu wa Rais Kamala Harris alivyoliambia shirika la utangazaji la CBS nchini Marekani hivi karibuni.

Soma zaidi: Uingereza yashinikizwa kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel

Akizungumzia kugeuka kwa kauli, Freilich anasema kuwa hivyo ndivyo unavyoweza kusema kuhusu utawala wa ovyo.

"Iwapo Netanyahu hatabadili msimamo wake hivi karibuni na ikiwa hakutakuwa na serikali mpya hivi karibuni, basi kutakuwa na athari ya kudumu," anasema mchambuzi huyo.

Ian Lustick, mtaalamu wa Israel na profesa wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Pennsylvania, aliiambia DW kwamba huu umekuwa mchakato wa kujivuta sana ambapo Marekani  imekuwa ikihama kutoka taa ya kijani hadi ya manjano na sasa ya machungwa.

Rangi ya machungwa ikimaanisha kutoshiriki kwa nchi hiyo katika kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hatua iliyowezesha kupitishwa kwa azimio la kusitishwa kwa muda kwa mapigano baada ya kushindwa kwa juhudi za awali.

Maandamano ya kupinga vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika jijini New York tarehe 28 Machi 2024.
Maandamano ya kupinga vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika jijini New York tarehe 28 Machi 2024.Picha: Andrew Kelly/REUTERS

Siasa kali chini ya Netanyahu
 

Kwa kujibu hatua hiyo, Netanyahu aliibua upinzani kuhusu ziara ya maafisa wa Israel nchini Marekani.

Bado serikali ya Biden imeidhinisha mauzo zaidi ya silaha kwa Israel tangu Oktoba 7 kama ilivyoripotiwa mara ya kwanza na gazeti la The Washington Post.
Soma zaidi: Israel yasema shambulizi lililowauwa wafanyakazi wa misaada lilikuwa "kosa kubwa"

Kwa miongo kadhaa, Israel imekuwa ikielekea zaidi upande wa kulia na watu wenye misimamo mikali ya kidini wamepata nguvu zaidi ya kisiasa, kwa kiasi kikubwa chini ya serikali tofauti za uongozi wa Netanyahu. 

Juhudi za Israel za kudumisha udhibiti dhidi ya Wapalestina zimeiweka Israel katika msuguano hasa na tawala za kidemokrasia. Mataifa hayo yamepishana nayo kuhusu masuala muhimu kama vile Iran, makaazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Palestina.

Utawala wa Marekani pia umeendelea kulaani idadi kubwa ya mauaji ya raia.

Msimamo wake kwa upana zaidi ni kuhusu hatua sawa za uhuru, fursa, na demokrasia kwa Waisraeli na Wapalestina. 

Hatua ya Israel ya kuteka maeneo zaidi ya Kipalestina, inahujumu maono hayo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Maya Alleruzzo/AP/dpa/picture alliance