1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stoltenberg: Hakuna mpango kuwapeleka wanajeshi Ukraine

30 Januari 2022

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg  amesema Jumuiya hiyo haina mpango wa kupeleka wanajeshi wa mapambano kwa taifa ambalo sio mwanachama wake ambae ni Ukraine, iwapo Urusi itaamua kuivamia.

https://p.dw.com/p/46Hnn
Belgien I Jens Stoltenberg I NATO
Picha: John Thys/AFP

Amesema kile wanachokitaka kwa sasa ni kuiunga mkono Ukraine na wala hawana nia ya kutuma wanajeshi wake huko. Stoltenberg ameongeza kuwa kuna tofauti kati ya kuwa mwanachama wa NATO na kuwa mshirika unayethaminiwa kama Ukraine.

Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Liz Truss amesema nchi yake wiki ijayo itaweka sheria mpya ya vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi kwa Urusi kama sehemu ya juhudi za kuizuiwia kuivamia ukraine. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uingereza amesema vikwazo hivyo vinalenga kuiwajibisha Urusi.

soma zaidi: Urusi na Belarus zajiandaa kwa luteka kubwa ya kijeshi

Waziri Truss ameonya kuwa wanachama wa Ulaya wanapaswa kuungana pamoja kuishinda nguvu Urusi na kuweka kipaumbele masuala ya utetezi wa uhuru na demokrasia. Uhusiano kati ya Urusi na Mataifa ya Magharibi umeyumba tangu vita baridi kufuatia Moscow kuweka maelfu ya wanajeshi wake mpakani mwa Ukraine.

Uingereza yapanga kuongeza wanajeshi zaidi NATO

Großbritannien | Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: House of Commons/PA via AP/picture alliance

Hatua hiyo imeendelea kuzua hofu ya taifa hilo kuivamia kijeshi Ukraine hali iliyoisababisha Jumuiya ya kujihami NATO na wanachama wake wa kimaeneo kufikiria kuweka wanajeshi wake huko. Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema wiki ijayo Uingereza inapanga kutoa wanajeshi, silaha na ndege za kivita katika Jumuiya hiyo.

Johnson alitangaza hayo jana Jumamosi kufuatia mzozo unaoendelea kati ya Urusi na nchi za magharibi kuhusu Ukraine huku akisema kwamba ongezeko hilo la wanajeshi litatuma ujumbe kwa rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba nchi za Magharibi hazitaruhusu matendo yake yanayotishia utulivu.

soma zaidi: Putin asema Marekani na NATO zimepuuza matakwa ya Urusi

Urusi imewarundika wanajeshi wake 100,000 karibu na mpaka wake na Ukraine, hali ambayo imezusha wasiwasi kwamba inapanga kuivamia Ukraine. Urusi imekanusha madai ya kupanga kuivamia Ukraine. Hapo jana ukraine iliiomba Jumuiya ya Kimataifa kubakia makini na thabiti katika mazungumzo yake na Urusi wakati rais wa Marekani Joe Biden akitangaza kuwapeleka wanajeshi kadhaa Mashariki mwa Ulaya kufuatia hofu hiyo ya uvamzi.

Chanzo: Reuters/AFP/AP