1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rudi Völler arefusha mkataba DFB

8 Aprili 2024

Shirikisho la soka la Ujerumani DFB, limetangaza kwamba Rudi Völler atasalia kuwa mkurugenzi wa timu za taifa za wanaume za Ujerumani hadi Kombe la Dunia la 2026.

https://p.dw.com/p/4eYOU
Ujerumani - Ufaransa
Rudi Völler mkurugenzi wa michezo timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani.Picha: Federico Gambarini/dpa/picture alliance

Völler, 63, mshambuliaji na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani alichukua kazi hii mpya iliyoundwa baada ya Ujerumani kuondolewa katika Kombe la Dunia la 2022 hatua ya makundi, kama sehemu ya kikosi kazi cha DFB kinachounda mabadiliko.

Timu ya taifa inayonolewa na Julian Nagelsmann sasa imeanza kuimarika baada ya kipindi kigumu, na Völler amehusishwa moja kwa moja na mabadiliko hayo.

"Pamoja na uzoefu wake wote, Rudi Völler ni muhimu na mshauri wangu na pia kwa makocha na wachezaji. Ana ushawishi chanya kwa timu ya taifa," alisema Rais wa DFB Bernd Neuendorf katika taarifa.

"Baada ya kipindi kigumu hivi karibuni, kuna mengi ya shauku kwa timu ya taifa tena. Mbali na kazi bora ya Julian Nagelsmann na timu yake, hii pia ni juhudi ya Rudi Völler." aliongeza Neuendorf.

Matokeo chanya

Kandanda
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Toni Kroos na Kai Havertz. Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Ujerumani ilirejea katika fomu yake mnamo Machi katika mechi za kirafiki na ushindi dhidi ya Ufaransa na Uholanzi, na DFB imesema ingependa kuongeza pia mkataba wa Nagelsmann ambao utaendelea hadi michuano ya Euro.

Völler alisema "Katika kipindi cha miezi 14 iliyopita ya kazi yangu, nimetambua

kwamba nimekua nikipenda zaidi na zaidi jukumu langu la uwajibikaji katika

DFB kila siku."

"Kama mkurugenzi wa timu ya taifa , ningependa kutumia uzoefu wangu, nataka kuchukua jukumu katika kuhakikisha kuwa timu bora ya taifa ya soka ya Ujerumani  imefanikiwa tena, lakini pia zaidi ya mafanikio ya nyumbani majira ya joto katika Michuano ya Ulaya.

Mustakabali wa Nagelmann

DFB Ufaransa - Ujerumani
Kocha wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani Julian Nagelsmann akitoa maagizo kwa wachezaji wake wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Ufaransa.Picha: BEAUTIFUL SPORTS/Wunderl/IMAGO

Kocha Nagelsmann amesema angependa hatma yake iamuliwe kabla ya

mashindano ya EURO, na anaweza kuendelea katika usukani wa timu ya taifa  Ujerumani au kurudi kwenye ukocha wa klabu.

"Pia tunatarajia kuongeza mkataba wake [Völler] kutuma ishara chanya

kwa kocha wa taifa Julian Nagelsmann, ambaye pia tunapenda kufanya kazi naye  kwa muda mrefu," mkurugenzi mkuu wa DFB Andreas Rettig alisema.

Völler aliichezea Ujerumani mara 90, akishinda Kombe la Dunia mwaka 1990 na

akicheza fainali za Kombe la Dunia 1986 na Euro 1992.

Alikuwa kocha wa Ujerumani na alitinga fainali ya Kombe la Dunia 2002 wakati wa uongozi wake 2000-2004, na alikuwa kocha wa muda kwa mechi moja mwaka jana kabla Nagelsmann kuchukua jukumu.

Kabla ya kibarua cha DFB alikuwa mkurugenzi wa michezo kwa muda mrefu

na mkurugenzi mkuu wa michezo katika klabu ya Bundesliga Bayer Leverkusen hadi 2022.