1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu akataa miito ya kusitishwa vita Gaza

Bruce Amani
4 Novemba 2023

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemwambia Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken kuwa Israel haina nia ya kukubali usitishwaji wa mapigano. Marekani inataka vita visitishwe ili misaada ifike Gaza

https://p.dw.com/p/4YOZY
Gazastreifen | israelischer Luftangriff auf einen Krankenwagen der von Hamas Kämpfern benutzt worden seien soll
Israel ilithibitisha kulishambulia gari la kuwabeba wagonjwa nje ya hospitali ya al-ShifaPicha: Momen Al-Halabi/AFP/Getty Images

Akizungumza baada ya kukutana na Blinken, Netanyahu amesema aliweka wazi kuwa wataendelea kusonga mbele kwa nguvu zote, na kwamba wanakataa usitishwaji wowote wa mapigano  ambao hautajumuisha kuwachiwa kwa mateka wao. Maafisa wa Israel wanakadiria kuwa karibu watu 249 walitekwa katika mashambulizi ya Oktoba saba na wanashikiliwa mateka Gaza.

Soma pia: UN yahitaji dola bilioni 1.2 kuwasaidia Wapalestina

Umoja wa Mataifa unazingatia usitishwaji wa mapigano kwa ajili ya kupelekwa misaada kuwa ni mpango wa muda mfupi unaofikiwa na pande zote ili misaada ifikishwe katika eneo maalum kwa muda maalum.

Na kusitishwa mapigano, kwa upande mwingine, ni mpango wa muda mrefu na haswa huwa sehemu ya mchakato wa kisiasa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri Blinken alikuwa Israel kabla ya kwenda JordanPicha: Jonathan Ernst/Pool Photo via AP/picture alliance

Blinken asisitiza kuhusu ulinzi wa raia wa Gaza

Awali waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alikutana na Rais wa Israel Isaac Herzog mjini Tel Aviv, akisisitiza kuwa Israel ina haki ya kujilinda, wakati akizungumzia haja ya kuongeza kwa kiasi kikubwa na haraka msaada endelevu katika Ukanda wa Gaza.

Blinken vilevile alisisitiza kuhusu ulinzi wa raia wa Gaza ambao wamenaswa katika makabiliano hayo yaliyochochewa na Hamas, akisisitiza kuwa kila kitu kifanywe kuwalinda na kupeleka msaada kwa wale wanaouhitaji kwa dharura na ambao kwa njia yoyote ile hawahusiki na matukio ya Oktoba saba.

Alipoulizwa kuhusu hotuba ya kiongozi mkuu wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah, Blinken alisisitiza kuwa Marekani imedhamiria kuhakikisha kuwa hakuna upande wa pili na wa tatu katika mzozo huo. Alisema Marekani iko katika hali ya tahadhari kubwa katika upande wa kaskazini, kujibu tukio lolote linaloweza kutokekea kwa sasa na katika siku zijazo kuhusiana na Lebanon, Hezbollah au Iran. Nasrallah alionya kuwa vita kati ya Israel na Hamas vinaweza kugeuka kuwa mzozo wa kikanda kama mashambulizi yataendelea Gaza.

Mtanziko wa Ujerumani juu ya azimio la Umoja wa Mataifa

Israel yashambulia gari la wagonjwa Gaza

Jeshi la Israel limesema moja ya ndege zake ilishambulia gari la kuwasafirisha wagonjwa katika mji wa Gaza jana. Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas ilisema shambulizi la Israel liliupiga msafara wa magari ya wagonjwa karibu na hospitali ya Al-Shifa, ambayo ndiyo kubwa kabisa katika ukanda huo.

Soma pia: Jeshi la Israel limetangaza kuuzingira kikamilifu Mji wa Gaza

Ilisema mlipuko huo uliwauwa watu 13 na kuwajeruhi 26. Msemaji wa jeshi la Israel alidai gari hilo la wagonjwa lilipigwa kwa sababu lilikuwa linatumiwa na wanamgambo wa Hamas. Madai hayo hayakuweza kuthibitishwa kwa njia huru.

Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limelaani tukio hilo likisema hospitali ya Al-Shifa kwa sasa inakumbwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa. WHO imesema msafara huo ulishambuliwa wakati ukisafirisha waliojeruhiwa kutoka hospitali hiyo ya Gaza kuelekea Rafah.

afp, ap, reuters, dpa