1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurundi

Ndayishimiye aituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa Burundi

29 Desemba 2023

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi ameituhumu kwa mara nyengine Rwanda kuwasaidia waasi wa Red Tabara wanaoishambulia mara kwa mara Burundi, tuhuma zinazozidisha uhasama kati ya mataifa hayo jirani.

https://p.dw.com/p/4aiGB
Burundi Bujumbura | Rais Evariste Ndayishimiye
Rais wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: Tchandrou Nitanga/AFP/Getty Images

Rais ameyasema hayo hivi leo akiwa kwenye mkutano na wananchi na waandishi wa habari, uliorushwa moja kwa moja na televisheni na redio ya taifa akiwa mkoani Cankunzo kwenye mpaka wa Burundi na Tanzania.

Rais huyo wa Burundi ameinyooshea kidole Rwanda kwa kile alichosema ni kuwasaidia kwa hali na maliwaasi hao wa Red Tabara, huku akielezea masikitiko yake kwamba juhudi zote za majadiliano na Rwanda juu ya suala hilo hazikufua dafu.

Alisema kwa takriban miaka miwili wamekuwa katika mazungumzo ili waasi hao warudishwe nchini Burundi, lakini hakuna muafaka uliofikiwa hadi sasa.

"Kama mnavyojuwa ndio waliohusika na janga la 2015. Kinachosikitisha ni kuwa tumeshindwa, kwani tungekuwa hatukushindwa wangetukubalia kuwarudisha nchini." Alisema

Aliongeza kuwa makundi hayo yanapewa hifadhi, mahitaji ya kiutu ikiwemo chakula, pesa za kutumia na nchi ya Rwanda na pahala salama kufanyia kazi zao.

Soma pia:Ndayishimiye ziarani Kinshasa kujadili amani, ushirikiano

Waasi hao walitajwa kuhusika na mauwaji na raia 20 na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa usiku wa tarehe 22 kuamkia 23 mwezi huu maeneo ya Gatumba karibu na mpaka mwa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Ama kuhusu taarifa kwamba baadhi ya wanajeshi wa Burundi waliopelekwa kusimamia usalama mashariki mwa Kongo wamekamatwa mateka, rais Ndayishimiye amekumbusha kuwa wanajeshi hao walipelekwa huko kufuatia mikataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kwamba kutekwa kwao hakutosababisha makubaliano hayo kusimama, kwani Burundi ilikubali kusaidia kukabiliana na ugaidi duniani.

Ndayishimiye azungumzia pia siasa ndani ya Burundi

Swala jingine lilochomoza katika mkutano huo uliowajumuisha wananchi wa kawaida na waandishi wa habari, ambao ulitoa fursa kwa kila mtu aliyetaka kumuuliza swali rais huyo wa Burundi moja kwa moja, ni mfarakano ndani ya chama kikuu cha upinzani cha CNL.

Rais Ndayishimiye amemshauri mkuu wa chama hicho, Agathon Rwasa, kuhakikisha jawabu linapatikana ndani ya chama hicho, na kuonya kuwa tofauti na hapo huenda kukawa na matokeo mabaya, ikiwemo kusambaratika kwa chama.

Vyama vya siasa vya upinzani Afrika vimetekeleza wajibu wao?

 "Nyumba isiyoacha kukabiliwa na malumbano hudharaulika, na utaanza kusema na walio nje ndio wanaokuja kuniharibia." Alisema kwa kutumia misemo ambayo imekuwa ikitumiwa na Warundi katika kufikisha ujumbe wa maridhiano palipo na changamoto.

Alizidi kuwaasa wanasiasa ndani ya chama hicho cha upinzani kuhakikishawanaondoa tofauti zao na kujenga chama chao ambacho kimekuwa na mchango mkubwa kwa demokrasia ya taifa hilo.

"Makundi mawili yanayohasimiana yote ni vigogo wa chama CNL. Neno la Mungu latufundisha kuwa ufalme usioungana husambaratika."

Soma pia:Kiongozi wa kijeshi wa Gabon ziarani Burundi

Rasi Ndayishimiye amejibu pia juu msimamo wa serikali yake  kuhusiana na ndoa za watu wa jinsia moja, akisema kwamba hakuna sababu za kujizolea laana na kwamba kamwe Burundi haitoruhusu kuwepo na sheria ya kuruhusu ndoa hizo.

Katika pindi hicho waandishi habari na hata raia wa kawaida wameuliza pia maswali juu ya uhaba wa maji, mafuta ya petroli, na pia suala la benki kuu ya Jamhuri kuwa chini ya mamlaka ya Ikulu ya rais.