1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Navalny akamatwa baada ya kutua Moscow

Bruce Amani
18 Januari 2021

Kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny amekamatwa katika uwanja wa ndege wa Moscow wakati akijaribu kuingia nchini humo akitokea Ujerumani, ambako aliishi miezi mitano akipata matibabu kutokana na tukio la kupewa sumu

https://p.dw.com/p/3o3RT
Russland Moskau | Flughafen Scheremetjewo | Alexej Nawalny
Picha: Kirill Kudryavtsev/AFP/Getty Images

Kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny alikamatwa jana katika uwanja wa ndege wa Moscow wakati akijaribu kuingia nchini humo akitokea Ujerumani, ambako aliishi miezi mitano akipata matibabu kutokana na tukio la kupewa sumu inayoathiri mishipa ya fahamu alilodai lilifanywa na serikali ya Urusi.

Kukamatwa kwa Navalny katika uwanja wa ndege wa Sheremtyevo mjini Moscow kulitarajiwa na wengi kwa sababu idara ya magereza ya Urusi ilisema alikiuka masharti ya kifungo chake kilichoahirishwa kutokana na hukumu aliyopewa 2013 ya ubadhirifu.

Idara ya Magereza imesema atawekwa kizuizini hadi mahakama itakapofanya uamuzi kuhusu kesi yake. Hakuna tarehe iliyotolewa ya mwanasiasa huyo kufikishwa mahakamani.

Navalny mwenye umri wa miaka 44, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais wa Urusi Vladmir Putin alipuuzilia mbali wasiwasi kuhusu kukamatwa kwake wakati alipopanda ndege mjini Berlin.