1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

NATO: Bakhmut huenda ikaanguka mikononi mwa Warusi

8 Machi 2023

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameonya kuwa mji wa Bakhmut, huenda ukaanguka mikononi mwa Warusi katika siku chache zijazo kufuatia miezi kadhaa ya mapigano makali.

https://p.dw.com/p/4OPCH
Schweden | NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Picha: Jonas Ekstromer/TT News Agency/AP/picture alliance

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameonya leo kuwa mji ulioharibiwa kabisa kwa vita wa mashariki mwa Ukraine, Bakhmut, huenda ukaanguka mikononi mwa Warusi katika siku chache zijazo kufuatia miezi kadhaa ya mapigano makali. Stoltenberg amewaambia waandishi habari mjini Stockholm pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya kuwa kinachoonekana kwa sasa ni kuwa Urusi inawapeleka wanajeshi zaidi, na hiyo inawaongeza nguvu za kuwakabili Waukraine.

Kampuni ya mamluki ya Urusi, Wagner, ilidai leo kuwa vikosi vyake vimekamata upande wa mashariki mwa Bakhmut, mji wa kiviwanda ambako mapigano kati ya wanajeshi wa Urusi na Ukraine yamerindima kwa miezi kadhaa. Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanajadili mipango ya kuimarisha uzalishaji wa zana za kivita na kupeleka kwa haraka nchini Ukraine kupambana na mashambulizi ya Urusi.