1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanahabari mashuhuri DRC ahukumiwa miezi 6 jela

Jean Noël Ba-Mweze
19 Machi 2024

Mwanahabari Stanis Bujakera nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anayeandikia jarida la Jeune Afrique pia mmoja wa viongozi wa gazeti la mtandaoni actualité.cd amehukumiwa jana kifungo cha miezi sita gerezani.

https://p.dw.com/p/4dtDg
Maandamano ya kushinikiza Stanis Bujakera kuachiwa huru
Waandishi wa habari wakiandamana Kongo kushinikiza kuachiwa kwa BujakeraPicha: Paul Lorgerie/DW

Stanis Bujakera amekuwa mbaroni tangu Septemba mwaka janaakituhumiwa kutengeneza na kutangaza ripoti kuhusu kifo cha mbunge Cherubin Okende ikidaiwa kuwa ni ya shirika la upelelezi la taifa, ANR. Mawakili wake walijaribu mara kadhaa kuomba aachiliwe kwa muda ila hawakufanikiwa.

Soma: Stanis Bujakera ni mwandishi wa habari mashuhuri na Kamerhe amesema wazi anamuunga mkono

Hatimaye mahakama kuu ya Kinshasa-Gombe ilimhukumu jana Jumatatu kifungo cha miezi sita jela na faini ya faranga milioni moja za Kongo ambazo ni takriban dola 370 za kimarekani. Lakini Bujakera lazima aondoke gerezani mara moja kwani tayari ameshatumikia kifungo hicho, kama alivyoeleza Charles Mushizi, mmoja wa mawakili wake.

Mawakili wa Stanis Bujakera
Mawakili wanaomtetea BujakeraPicha: Paul Lorgerie/DW

"Sheria inamruhusu kuhesabu muda huo ili kurudishiwa uhuru wake mara moja kwani alihukumiwa kifungo cha miezi sita ambapo tayari ameshakaa gerezani ingawa alipata adhabu ambayo ingeliepukikiwa. Kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kuachiliwa kwake na hivyo siku za usoni anaweza kukata rufaa kama akitaka."

Hukumu wa Bujakera ilitolewa saa chache tu baada ya miungano ya wanahabari  kukutana Jumatatu hiyo hiyo mjini Kinshasa na kuitisha maandamano ili kudai aachiliwe. Na hivi tayari amehukumiwa ingawa ataachiliwa punde, baadhi ya miungano hiyo imekosoa na kutupilia mbali uamuzi huo na kumhimiza Bujakera kukata rufaa. Edmond Izuba ni kiongozi wa muungano RAJEC.

"Tunaendelea kudai kuachiliwa kwa Bujakera tukitupilia hukumu hiyo kwani hajui chochote kuhusu kesi hiyo. Tunamhimiza kukata rufaa ili kuonyesha kwamba hana hatia yoyote. Hukumu hiyo inafanana na mpangilio wa kisiasa."

Mwendesha mashtaka mkuu alikuwa ameomba kifungo cha miaka ishirini  dhidi ya Bujakera lakini hakukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa. Wanahabari hapa Kongo wanahofia mkakati wa mamlaka ya Kongo kujaribu kuwanyamazisha.