1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Wagner ahamia Belarus, NATO yaapa kulinda washirika

Bruce Amani
28 Juni 2023

Belarus imemkaribisha mkuu wa kundi la mamluki wa kijeshi la Wagner, Yevgeny Prigozhin uhamishoni jana Jumanne, kufuatia uasi uliotibuka wakati jumuiya ya NATO ikionya kuwa iko tayari kujilinda dhidi ya Urusi au Belarus.

https://p.dw.com/p/4T9u6
Yevgeny Prigozhin
Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner Yevgeny Prigozhin.Picha: AP/picture alliance

Rais wa Urusi Vladmir Putin alijaribu kuimarisha mamlaka yake kufuatia uasi huo uliotikisa nafasi yake, kwa kuwashukuru wanajeshi wa kawaida kwa kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Lakini wakati Moscow ikitangaza mipango ya kuapokonya silaha wapiganaji wa Wagner, mpinzani mkuu wa Putin Alexei Navalny, amemkosoa vikali kiongozi huyo na kuutaja utawala wake kuwa ndiyo kitisho kikubwa zaidi kwa Urusi.

Mjini The Hague, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO Jens Stoltenberg alisema ilikuwa bado ni mapema mno kutoa mahitimisho kutokana na kuhamia kwa Prigozhin nchini Belarus, lakini aliapa kwamba muungano huo uko tayari kuwalinda wanachama wake.