1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Meli ya shehena ya misaada yang'oa nanga Cyprus kuenda Gaza

John Juma
9 Mei 2024

Shehena ya misaada imeondoka Cyprus na tayari iko njiani kuelekea Gaza. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya nje wa Cyprus Constantinos Kombos.

https://p.dw.com/p/4fg47
Umoja wa Mataifa umesema raia wa gaza wako katika ukingo wa kutumbukia kwenye baa la njaa.
Umoja wa Mataifa umesema raia wa gaza wako katika ukingo wa kutumbukia kwenye baa la njaa.Picha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Msaada huo unasafirishwa mnamo wakati Umoja wa Mataifa umesema watu wa Gaza wako katika ukingo wa kutumbukia kwenye baa la njaa, na hasa baada ya vikosi vya Israel kuwataka takriban wakaazi 100,000 wa kusini mwa Gaza kuondoka katika mji wa Rafah.

Mapema wiki hii, Israel ilipeleka vifaru vyake vya kivita kukamata kivuko cha karibu kati ya Rafah na Misri, na kufunga mpaka huo muhimu ili iweze kutimiza lengo lake la kuliangamiza kundi la Hamas, baada ya shambulizi lake la Oktoba 7, kusini mwa Israel.

Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 1,200 na wengine 250 walichukuliwa mateka na kupelekwa Gaza.

WHO: Hospitali za Rafah kukosa mafuta ndani ya siku tatu

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Marekani ambayo inapinga operesheni ya Israel mjini Rafah imesema Israel haijatoa utaratibu wa kuwaondoa na kuwalinda raia waliokimbilia Rafah.

Kulingana na maafisa wa wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, vita vya Gaza vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 34,800, na takriban asilimia 80 ya idadi jumla ya Wapalestina milioni 2.3 wameyakimbia makwao.

Upakuaji wa shehena ya misaada kwenye meli ukiendelea katika bandari ya Larnaca Cyprus mnamo Machi 15, 2024.
Upakuaji wa shehena ya misaada kwenye meli ukiendelea katika bandari ya Larnaca Cyprus mnamo Machi 15, 2024.Picha: Petros Karadjias/AP Photo/picture alliance

Biden atishia kutoipa Israel silaha

Mnamo Jumatano, rais wa Marekani Joe Biden, alisema hataipa Israel silaha inayoweza kutumia kushambulia Rafah.

Wapalestina waukimbia mji wa Rafah kabla ya mashambulizi ya ardhini

Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani CNN, Biden alisema angali amejitolea kuipa Israel mifumo ya kuzuia makombora na zana nyingine za kujilinda lakini sio silaha za kushambulia.

Kauli ya Biden imekosolewa na baadhi ya viongozi wa Israel.

Itamar Ben Gvir, waziri wa Usalama wa Taifa nchini Israel na anayeegemea siasa kali za mrengo wa kulia, aliashiria kwamba Hamas wanampenda Biden, akitumia emoji ya mchoro wa moyo kwenye ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake wa X.

Israel yafungua tena kivuko mpakani kati ya Gaza na Misri

Katika tukio jingine, Waziri wa mambo ya Nje wa Cyprus Constantinos Kombos amesema meli ya Marekani ambayo imebeba shehena ya msaada wa kiutu unaohitajika sana, imeondoka Cyprus kuelekea Gaza.

Waziri wa mambo ya Nje wa Cyprus ​​Constantinos Kombos akimkaribisha mwenzake wa Israel Eli Cohen mjini Larnaca Cyprus mnamo Disemba 20, 2023.
Waziri wa mambo ya Nje wa Cyprus ​​Constantinos Kombos akimkaribisha mwenzake wa Israel Eli Cohen mjini Larnaca Cyprus mnamo Disemba 20, 2023.Picha: Stavros Ioannides/PIO/Handout via REUTERS

Bandari iliyotengenezwa pwani ya Gaza kuanza kupokea shehena

Shehena hiyo itakuwa ya kwanza kupokelewa kwenye bandari mpya iliyojengwa maili kadhaa pwani ya Gaza kama njia mbadala badala ya Barabara ambayo Israel imewekea vikwazo vingi.

Mnamo Jumatano, mashirika ya kimataifa ya misaada yalionya kuwa mtandao wa usambazaji misaada upo katika hatari ya kuporomoka katika eneo lote kwa sababu usafirishaji wa mafuta kuingia Gaza umekatika.

Mashirika hayo yamesema kitisho cha Israeli cha kuivamia Rafah yenyewe, ambapo makundi mengi ya misaada yameweka maghala na wafanyakazi wao, pia inatatiza zaidi usambazaji misaada.

Vyanzo: DPAE, APAE