1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin akutana na Erdogan mjini Sochi

4 Septemba 2023

Mazungumzo yaliyofanyika mjini Sochi kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan kuhusu Mkataba wa usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi yamemalizika baada ya saa tatu.

https://p.dw.com/p/4Vwnk
Russland Sotschi Türkei Erdogan Putin
Picha: Sergei Guneev/Sputnik/REUTERS

Taarifa za kuhitimishwa kwa mazungumzo hayo muhimu kati ya Putin na Erdogan imetolewa na shirika la habari la serikali ya Urusi TASS huku msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov akisema kuwa sehemu ya kwanza ya mazungumzo hayo yalikuwa yenye tija.

Hata hivyo shirika jengine la habari la serikali ya Urusi RIA limeripoti kwamba Peskov amebaini kuwa hakuna tamko la pamoja linalotarajiwa baada ya kumalizika mazungumzo hayo.

Rais wa Uturuki  Recep Tayyip Erdogan  alidhamiria licha ya vita kuendelea, kumshawishi Rais wa Urusi Vladimir Putin kufufua makubaliano ambayo yaliruhusu usafirishaji na uuzaji wa nafaka na bidhaa nyingine za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi.

Donau-Hafen Ismajil
Meli ya usafirishaji nafaka katika mji wa Izmail nchini Ukraine: 26.04.2023Picha: Andrew Kravchenko/AP Photo/picture alliance

Erdogan amesema mpango huo wa nafaka ndio ajenda kuu iliyotawala mazungumzo hayo katika makaazi ya mapumziko ya rais Putin mjini Sochi nchini Urusi.

Soma pia: Erdogan kumshawishi Putin kufufua mkataba wa nafaka Ukraine

Putin amebaini kwamba mazungumzo na Erdogan yaligubika uhusiano wa kibiashara lakini pia maswala yanayohusiana na mzozo wa Ukraine:

" Karibu Urusi na hapa Sochi. Tuliafikiana juu ya mkutano huu muda mrefu uliopita, lakini baada ya uchaguzi nchini Uturuki, huu ni mkutano wetu wa kwanza. Nina furaha kukupongeza kwa matokeo. Tuna mengi ya kuzungumza juu ya mtazamo wa kuhakikisha usalama katika kanda zima. Bila shaka, hatutapuuza masuala yanayohusiana na mgogoro wa Ukraine. Ama kuhusu mpango wa usafirishaji nafaka, tuko tayari kwa mazungumzo juu ya suala hili. "

Urusi kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Uturuki

Russland Sotschi Türkei Erdogan Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) akimpokea Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Sochi, Urusi 04.09.2023Picha: Alexei Nikolsky/AP Photo/picture alliance

Licha ya Urusi kujiondoa katika mkataba huo, Putin amesema Moscow inakaribia kufikia makubaliano yatakayopelekea mauzo ya nafaka bila malipo kutoka Urusi hadi nchi sita za Afrika.

Erdogan amekuwa akiahidi mara kwa mara kuwa atahakikisha ana ufufua mkataba huo ambao ulisaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia mgogoro wa chakula duniani hasa katika mataifa ya Afrika Asia na Mashariki ya Kati.

Soma pia: Putin kukutana na Erdogan leo kujadili makubaliano ya nafaka

Aidha, Rais wa Uturuki amesema serikali yake inalenga kukuza uhusiano wa kibiashara wa kila mwaka na Urusi hadi kufikia dola bilioni 100 kutoka dola bilioni 62, akiongeza kwamba anaunga mkono msukumo wa Moscow wa kufanikisha sehemu ya biashara hiyo kwa kutumia sarafu za mataifa hayo mawili.

Rais wa Uturuki amedumisha uhusiano wa karibu na Putin katika kipindi cha miezi 18 tangu urusi ilipoivamia Ukraine. Ankara haijaunga mkono vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow kufuatia uvamizi huo, na hivyo kuwa mshirika wake mkuu wa kibiashara.