1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya waijadili hali ya Gaza

22 Januari 2024

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wamekutana kwa mazungumzo na viongozi wa Israel na wale wa Mamlaka ya Palestina mjini Brussels, Ubelgiji, huku vita vikiendelea huko Gaza na idadi ya vifo ikiongezeka.

https://p.dw.com/p/4bYSk
Brussels- Israel Katz akiwasili katika mkutano wa Mawaziri wa EU
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz (kulia) akiwasili katika mkutano huo wa Mawaziri wa mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels nchini Ubelgiji.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwa mazungumzo na wanadiplomasia wakuu kutoka mataifa muhimu ya kiarabu wakiwemo pia viongozi kutoka Israel na Palestina.

Mawaziri hao wameishinikiza hii leo serikali mjini Tel-Aviv kuafiki suluhu ya mataifa mawili baada ya vita huko Gaza na kusisitiza kuwa hiyo ndio njia pekee na ya kuaminika itakayowezesha kupatikana kwa amani katika eneo la Mashariki ya Kati. Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan na Saudi Arabia wanashiriki pia mazungumzo hayo na mawaziri wa Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Abdullah bin Abdul Rahman Al Hussein amesema:

" Tunatarajia msimamo thabiti kutoka kwa wenzetu wa Umoja wa Ulaya. Msimamo utakaokuwa upande wa amani, upande wa sheria za kimataifa, upande wa haki, wa kudai kusitishwa kwa mapigano, kufanya kazi pamoja nasi ili kuruhusu misaada ya kutosha ya kibinadamu kuingia Gaza na pia kushirikiana nasi katika mpango ambao utaleta amani ambayo kila mtu katika eneo anastahili."

Israel yaendelea kukaidi miito ya suluhu la mataifa mawili

Tel Aviv | Rais Joe Biden akiwa na Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kulia) akiwa na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Tel Aviv: 18.10.2023Picha: Brendan Smialowski/AFP

Israel hadi sasa imetupilia mbali miito hiyo ya kuwepo kwa taifa huru la Palestina na kusisitiza kuwa wataendelea kuwa na udhibiti huko Gaza hata baada ya vita hivyo kumalizika. Saudi Arabia imesema hii leo kuwa kamwe haitoitambua Israel endapo haitaafiki uwepo wa taifa huru la Palestina.

Soma pia: Israel yatofautiana na Marekani kuhusu kuundwa taifa la Palestina

Mustakabali wa Gaza na hata eneo zima la Palestina, umekuwa kiini cha mvutano baina ya Israel na mataifa mengi duniani ikiwemo pia mshirika wake mkuu Marekani ambaye amesisitiza mara kadhaa kuunga mkono suluhu la mataifa mawili.

Mapambano yaendelea huko Gaza

Gaza- Mashambulizi katika kambi ya Wakimbizi ya Jabalia
Wapalestina wakitembea karibu ya jengo lililoharibiwa na shambulizi la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza: 19.01.2024Picha: Xinhua/IMAGO

Mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Khan Younis umeendelea kushambuliwa na vikosi vya Israel leo Jumatatu ambapo Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas imesema kuanzia usiku wa jana, watu 50 wameuawa na wengine 100 wamejeruhiwa eneo hilo. Wizara hiyo imesema kufikia sasa watu zaidi ya 25,200 wameuawa huko Palestina.

Waziri Mkuu wa Israel  Benjamin Netanyahu anakabiliwa pia na shinikizo linaloongezeka la ndugu na jamaa wa mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas.  Familia za mateka hao wamekuwa wakikita kambi nje ya ya jengo la Bunge na pia karibu na makazi ya Netanyahu. Hii leo, kundi la karibu watu 20 wamevamia kikao cha kamati ya Bunge mjini Jerusalem na kusema wanaomba wapendwa wao waachiliwe huru.

(Vyanzo: Mashirika)