1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa kadhaa washambuliwa Ujerumani

Saumu Mwasimba
5 Mei 2024

Waziri wa mambo ya ndani Nancy Faeser aitisha mkutano na mawaziri wenzake wa majimbo 16 kujadili kadhia hiyo wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/4fWQ1
Bango la Matthias Ecke mjini Dresden
Bango la mwanasiasa wa SPD Matthias EckePicha: Robert Michael/dpa/picture alliance

Nchini Ujerumani yameitishwa maandamano ya kulaani mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa dhidi ya wanasiasa kadhaa pamoja na watu wanaofanya harakati za kampeni za uchaguzi wa Umoja wa Ulaya ndani ya Ujerumani.

Mashambulizi hayo ambayo yamekuwa yakiendelea kushuhudiwa katika mitaa mbali mbali yamesababisha mshtuko nchini Ujerumani.

Waziri wa mambo ya ndani Nancy Faeser ameitisha mkutano wa dharura na mawaziri wenzake wa ngazi za majimbo kuzungumzia hatua ya kuimarisha usalama ili kuzuia vurugu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya.

Baadhi ya matukio yaliyoripotiwa

Matthias Ecke,mwanasiasa wa chama cha Social Democrat (SPD) ambaye pia ni mbunge katika bunge la Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2022, alipigwa vibaya na genge la watu wanne siku ya Ijumaa wakati akiwa katika harakati zake za kubandika picha za kampeni katika mji wa Mashariki mwa Ujerumani wa Dresden. Kansela Olaf Scholz amelaani tukio hilo.

Kansela  Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa polisi, muda mfupi kabla ya Ecke kushambuliwa, kundi la watu wanne wasiojulikana walimshambulia mfanyakampeni mmoja wa chama cha Kijani mwenye umri wa miaka 28  wakati akibandika picha katika eneo hilohilo la Dresen. 

Kundi lililomshambulia mwanasiasa wa SPD, Ecke, kwa mujibu wa polisi linahusisha vijana wanne wa umri wa kati ya miaka 17 na 20.

Msemaji wa polisi amefahamisha kwamba shahidi mmoja ameeleza kwamba vijana hao walionekana kuwa sehemu ya mtandao wa wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia.

Bado polisi  wanaendelea kuchunguza uhalifu huo na hawajawakamata washukiwa.

Waziri wa mambo ya ndani Nancy Faeser
Waziri wa mambo ya ndani- Nancy FaeserPicha: Michal Cizek/AFP/Getty Images

Kumekuweko na matukio mengi katika kipindi hiki cha kampeni kote ndani ya Ujerumani ikiwemo tukio lililoripotiwa Alhamisi jioni katika mji wa Essen, Magharibi mwa Ujerumani ambako mbunge mmoja kutoka chama cha Kijani Kai Gehring na mwanachama mwenzie Rolf Fliss walishambuliwa baada ya kushiriki tukio moja la chama.

Lakini pia katika mji mwingine wa Magharibi mwa Ujerumani wa Nordhorn, mwanasiasa kutoka chama cha siasa kali kisichotaka wageni nchini Ujerumani cha AfD  alipata kipigo siku ya Jumamosi, akiwa katika kituo kimoja cha kupata taarifa, kwa mujibu wa polisi.

Bunge la Ulaya-Brussels
Bunge la Umoja wa UlayaPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Makundi mawili ya wanaharakati yameitisha maandamano Jumapili hii katika miji ya Dresden na Berlin kulaani vurugu hizo.

Mawaziri wa mambo ya ndani wa majimbo yote 16 ya Ujerumani wanatarajiwa kukutana wiki ijayo kuzungumzia juu ya matukio hayo. Waziri wa mambo ya nje Annalena Baerbock pia ametoa tamko kulaani mashambulio hayo.