1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Makamu Kansela wa Ujerumani afanya ziara ya ghafla Ukraine.

Zainab Aziz
3 Aprili 2023

Makamu wa Kansela wa Ujerumani Robert Habeck amefanya ziara ya ghafla nchini Ukraine. Pia watu 6 wamekufa, na wengine 10 wamejeruhiwa katika shambulio la makombora ya Urusi karibu na mji wa Bakhmut.

https://p.dw.com/p/4Pd5m
Vizekanzler Habeck in der Ukraine
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Makamu wa Kansela Robert Habeck ambaye pia ni waziri wa uchumi wa Ujerumani, aliwasili mjini Kyiv katika ziara ya ghafla leo Jumatatu asubuhi kwa mazungumzo ya kisiasa na mamlaka ya Ukraine. Habeck amesema lengo la mazungumzo hayo ni kuipa Ukraine matumaini kwamba nchi hiyo itajengwa upya baada ya vita. Kwenye mazungumzo hayo pande hizo mbili zitazingatia ushirikiano katika kuiendeleza upya miundombinu ya nishati ya Ukraine.

Makamu wa Kansela Robert Habeck ambaye pia ni Waziri wa Uchumi wa Ujerumani.
Makamu wa Kansela Robert Habeck ambaye pia ni Waziri wa Uchumi wa Ujerumani.Picha: Martin Schutt/picture alliance/dpa

Makamu wa Kansela wa Ujerumani Robert Habeck, amesema maamuzi ya uwekezaji yanapaswa kufanyika. Kiongozi huyo ameandamana na ujumbe wa wafanyabiashara wanaoendesha biashara za ukubwa wa wastani pamoja na rais wa Shirikisho la Viwanda nchini Ujerumani, Siegfried Russwurm.

Wakati huo huo nchini Ukraine, mkuu wa itifaki katika serikali ya rais Volodymyr Zelenskyy amesema watu wapatao sita wameuawa katika mashambulizi ya makombora ya Urusi kwenye eneo la makazi mashariki mwa nchi hiyo. Watu wengine wanane wamejeruhiwa. Mashambulio hayo yaliulenga mji wa Kostiantynivka ulio umbali wa kilomita 20 kutoka mji unaokabiliwa na mapigano wa Bakhmut katika eneo la Donetsk.

Mkuu huyo wa itifaki Andriy Yermak amesema kuwa mashambulizi makubwa ya makombora ya vikosi vya Urusi yamesababisha yameharibu majengo 16 ya ghorofa, nyumba nane za kibinafsi, shule ya chekechea na jengo la utawala katika mji huo.

Vita vya nchini Ukraine katika eneo la Bakhmut
Vita vya nchini Ukraine katika eneo la BakhmutPicha: Cover-Images/IMAGO

Kwingineko polisi nchini Urusi wanamshikilia mwanamke mmoja anayeshukiwa kuhusika na bomu lililomuua mwanabloga maarufu wa habari za kijeshi nchini Uurusi.  Mwanamke huyo anayeitwa Darya Trepova alitambuliwa na baadhi ya vyombo vya habari vya Urusi kwenye mitandao kama ndiye mshukiwa.

Maafisa wa Urusi wamesema mwanabloga huyo Vladlen Tatarsky,mwenye umri wa miaka  40, aliuawa Jumapili wakati akiongoza mjadala katika mkahawa mmoja kwenye kingo za Mto Neva katikati ya eneo la kihistoria la St Petersnurg. Kulingana na mamlaka, zaidi ya watu 30 walijeruhiwa katika mlipuko huo na 10 kati yao wamo katika hali mahututi. Ripoti zinaeleza kwamba bomu hilo lilifichwa kwenye sanamu ya kichwa hadi mabegani ya mfano wa mwanabloga huyo ambaye mshukiwa alimpa kama zawadi muda mfupi kabla ya kutokea mlipuko huo.

Marehemu mwanabloga wa Urusi Vladlen Tatarsky.
Marehemu mwanabloga wa Urusi Vladlen Tatarsky.Picha: Telegram @Vladlentatarskybooks/via REUTERS

Vladlen Tatarsky, ambaye jina lake halisi ni Maxim Fomin alikuwa na wafuasi 560,000 kwenye mtandao wa Telegram na alikuwa mmoja wa wanabloga mashuhuri walioandika kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine. Alikuwa mfuasi mkubwa wa Urusi katika vita hivyo vya nchini Ukraine.  Lakini pia, alikosoa kile alichokiona kama kushindwa kwa makamanda wa juu ya kijeshi.

Kutokana na kifo cha Tatarsky, msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova amesema shughuli za  mwanabloga huyo zimemsababishia chuki kutoka kwa serikali ya Ukraine na amebainisha kuwa marehemu Tatarsky na wanabloga wengine wanaoandika habari za kijeshi wa nchini Urusi kwa muda mrefu wamekuwa wanakabiliwa na vitisho vya Ukraine.

Vyanzo: DPA/AFP/AP