1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magavana Kenya kuchukua hatua dhidi ya mgomo wa madaktari

16 Aprili 2024

Mgomo wa madaktari nchini Kenya umechukua sura mpya baada ya magavana kutishia kuwachukulia hatua za sheria ya ajira, huku tume ya haki za binadamu ikitoa wito madaktari kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

https://p.dw.com/p/4erGQ
Kenia Demo der Ärzte in Nairobi - Vertretter der KMPDU festgenommen
Madaktari wakiwa katika mgomo nchini KenyaPicha: Reuters/T. Mukoya

Wakimiminika barabarani jijini Nairobi, madaktari na matabibu waliandamana guu mosi guu pili hadi ofisi za baraza la magavana. Madaktari hao wametoa ilani ya kuandamana kila Jumanne hadi pale kilio chao kitakaposikilizwa.

Kwenye kikao maalum cha baraza la magavana, mwenyekiti, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amebainisha kuwa ijapokuwa madaktari wana haki ya kugoma, kama waajiri wao hawana budi kufikia mwafaka.

Gavana Waiguru anasisitiza kuwa kama waajiri wa madaktari wa hospitali za umma wanalazimika kuchukua hatua zinazoendana na sheria za ajira ili kuwanusuru wagonjwa.

Soma pia:Madaktari wakataa pendekezo la kusitisha mgomo Kenya

Ifahamike kuwa mahakama inasuburiwa kutoa mwelekeo tarehe Aprili 17, 2024 baada ya kuwapa wadau wiki mbili za ziada kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya suluhu.

Kwa upande wake, waziri wa afya wa Kenya, Susan Nakhumicha anasisitiza kuwa wanafanya kila lililo ndani ya uwezo wao kufikia mwafaka. Kauli hizo zinaungwa mkono na mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro anayewarai madaktari kurejea kazini wakati suluhu inasakwa.

Akiwa katika kaunti ya Kajiado alielezea kuwa azma yao ni kupata suluhu ya kudumu wala sio ya muda mfupi.

Wauguzi kujiungana na madaktari katika mgomo

Wauguzi nao wanajiandaa kujiunga na mgomo na msimamo wao ni kuwa walipwe kwanza ndio wapange mikakati ya kurejea kazini bila vikwazo. Seth Panyako ni katibu mkuu wa muungano wa wahudumu, KNUN.

Yote hayo yakiendelea, tume ya Taifa kutetea haki za binadamu inatoa wito wa kusitisha vitisho kwa madaktari wanaogoma na kuuirai serikali kukaa nao kwenye meza ya mazungumzo.

Matumizi ya akili ya kubuni katika sekta ya afya Ujerumani

Soma pia:Serikali ya Kenya yawataka madaktari kusitisha mgomo wao

Wizara ya afya ya Kenya imependekeza madaktari wanafunzi kupewa shilingi alfu 70 za Kenya wanaponoa ujuzi wao kwenye hospitali za umma. Mpango huo utaigharimu serikali shilingi bilioni 2.4.

Hata hivyo, madaktari wenyewe kupitia Chama chao cha KMPDU wanadai walipwe shilingi laki mbili za Kenya kiasi ambacho ni maradufu ya kile kinachopangwa na serikali.

Serikali kupitia tume ya kuratibu mshahara, SRC, iliyo mwenyeji wa kongamano la tatu la mshahara la kitaifa linanoendelea, inakusudia kupunguza malipo ya umma.