1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinachoendelea Sudan kinatisha - Guterres

Iddi Ssessanga
9 Februari 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameihimiza jumuiya ya kimataifa kujipanga na kufanya kila kinachowezekana kukomesha vita nchini Sudan, akisema kinachoendelea huko kinatisha.

https://p.dw.com/p/4cDJP
Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.Picha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Katibu Mkuu Guterres alisema jana Alamisi kwamba hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo kati ya vikosi vinavyowaunga mkono majenerali hasimu, ambao ulianza katikati mwa Aprili 2023, na kusisitiza kuwa kuendelea kwa mapigano hakutaleta suluhisho lolote.

Soma zaidi: Ujumbe wa UN watakiwa kumaliza shughuli zake Sudan

Guterres aliuambia mkutano wa habari wa Umoja wa Mataifa hapo jana kwamba wakati umefika kwa mahasimu wa Sudan - Jenerali Abdel Fattah Burhan, na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, kuanza mazungumzo juu ya kumaliza mzozo, ambao umeua watu wasiopungua 12,000 na kuwalazimu zaidi ya milioni 7 kuyakimbia makazi yao.