1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUswidi

Jenerali wa zamani Syria kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita

Bruce Amani
15 Aprili 2024

Afisa wa ngazi ya juu zaidi katika jeshi la Syria kushitakiwa barani Ulaya atafikishwa katika mahakama moja ya Stockholm Jumatatu kwa madai ya kuhusika katika uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/4ekoz
Askari wa Syria katika mkoa wa Hama
Wanajeshi wa Syria wanatuhumiwa kwa mauaji ya raia katika mkoa wa Hama wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Picha: Xinhua/IMAGO

Brigedia jenerali wa zamani wa Syria Mohammed Hamo mwenye umri wa miaka 65, anayeishi Sweden, anatuhumiwa kwa kusaidia na kuunga mkono uhalifu wa kivita wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, mashitaka ambayo yanaweza kuwa adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Vita vya nchini Syria kati ya utawala wa Bashar al-Assad na makundi ya silaha ya upinzani, likiwemo Dola la Kiislamu, vilizuka baada ya serikali kukandamiza maandamano ya amani ya kuunga mkono demokrasia mwaka wa 2011. Vimewauwa zaidi ya watu nusu milioni, kuwaacha mamilioni ya wengine bila makazi na kuharibu kabisa uchumi na miundombinu ya nchi hiyo.

kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Hamo alichangia -- kupitia ushauri na vitendo kwa vita vya jeshi la Syria, vilivyohusisha mashambulizi ya kiholela kwenye miji kadhaa au maeneo ya ndani na karibu na miji ya Hama na Homs.

Waendesha mashitaka wanasema vita vya jeshi la Syria vinajumuisha mashambulizi ya anga na ardhini yaliyofanywa na wahusika wasiojulikana ndani ya jeshi la Syria. Walalamikaji kadhaa wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo, wakiwemo Wasyria kutoka miji iliyotajwa na mpiga mpicha Muingereza aliyejeruhiwa katika mojawapo ya mashambulizi.