1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yawataka raia wake kuondoka nchini Misri na Jordan

Tatu Karema
21 Oktoba 2023

Israel imewataka raia wake kuondoka nchini Misri na Jordan mara moja. Haya yamesemwa leo na baraza la usalama wa kitaifa la nchi hiyo wakati mvutano wa kikanda ukipamba moto kutokana na vita katika ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4XqXx
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Chad J. McNeeley/AA/picture alliance

Katika taarifa yake, baraza hilo limetoa tahadhari ya juu ya safari kuelekea nchini Misri hii ikijumuisha eneo la Sinai na pia Jordan na kushauri wale wanaoishi katika maeneo hayo kuondoka haraka iwezekanavyo.

Ilani hiyo inakuja siku chache baada ya Israel kuwarejesha nyumbani wanadiplomasia wake kutoka Uturuki kama tahadhari ya kiusalama kufuatia ombi la awali kwa raia wake pia kuondoka nchini humo.

Soma pia: Hamas yawaachia mateka wawili iliokuwa ikiwashikilia

Vita vinavyoendelea ni matokeo ya shambulizi baya kabisa lililofanywa ndani ya ardhi ya Israel na Kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza ambalo Israel na mataifa kadhaa ya magharibi yameliorodhesha kuwa la kigaidi.

Kulingana na maafisa wa Israel shambulizi hilo la Oktoba 7 lilisababisha vifo vya watu 1,400 na wengine zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.