1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kuitwanga Khan Younis

Zainab Aziz
24 Januari 2024

Majeshi ya Israel yamepambana na wapiganaji wa kundi la Hamas karibu na hospitali kuu katika mji wa Khan Younis, ambao ni wa pili kwa ukubwa kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4bcGp
Ukanda wa Gaza | Khan Yunis
Moshi ukifuka kutoka majengo yanayoporomoshwa kwa makombora ya Israel katika mji wa Khan Yunis, wa pili kwa ukubwa katika Ukanda wa Gaza.Picha: AFP/Getty Images

Wahudumu kwenye hospitali hiyo wamesema mamia ya wagonjwa na maelfu ya wakimbizi wa ndani hawakuweza kuondoka kutokana na mapigano.

Israel imewaamuru wakaazi wa sehemu hiyo ya Khan Younis inayojumuisha kitongoji cha Nasser na hospitali mbili ndogo kuondoka, wakati majeshi yake yakisonga mbele katika mapigano dhidi ya Hamas ambayo yameshachukua muda wa miezi mitatu.

Umoja  wa Mataifa umesema sehemu hiyo ilikuwa makaazi ya Wapalestina 88,000 na pia ilikuwa hifadhi ya watu wengine 425,000 waliopoteza makaazi yao kutokana na  mapigano.

Israel imesema majeshi yake yanapambana na Hamas ndani ya mji wa Khan Younis baada ya kukamilisha kuuzingira mji huo hapo jana.