1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yalaani mashambulizi ya Uturuki

Grace Kabogo
19 Septemba 2023

Ofisi ya Rais wa Iraq imelaani mashambulizi ya mara kwa mara ya Uturuki, siku moja baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia kwenye uwanja wa ndege wa Arbat na kuwaua maafisa watatu wa Kikurdi wanaopambana na ugaidi.

https://p.dw.com/p/4WZ0M
Syrien  Deir Ezzor
Picha: ZUMAPRESS.com/picture alliance

Ofisi hiyo imesema leo kuwa balozi wa Uturuki ataitwa kwa ajili ya kukabidhiwa barua inayopaswa kupelekwa kwa Rais Recep Tayyip Erdogan, kupinga mashambulizi hayo.

Msemaji wa kamanda mkuu wa jeshi la shirikisho, Jenerali Yehya Rassoul, amesema ndege hiyo ilitokea Uturuki.

Jenerali Rassoul amesema shambulizi hilo linakiuka uhuru wa Iraq, na nchi hiyo ina haki ya kukomesha ukiukaji huo.

Amesema mashambulizi hayo ya mara kwa mara hayaendani na kanuni ya ujirani mwema kati ya mataifa, na yanatishia kudhoofisha juhudi za Iraq kujenga uhusiano mzuri na wenye uwiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama na jirani zake.