1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaapa kujibu mashambulizi kama itashambuliwa

Mohammed Khelef
2 Februari 2024

Iran imeapa kujibu mashambulizi yoyote dhidi yake, wakati wasiwasi ukiongezeka kwamba huenda Washington ikaishambulia Tehran kulipiza kisasi mauaji ya wanajeshi wake watatu nchini Jordan.

https://p.dw.com/p/4byY4
Iran, Tehran | Ebrahim Raisi
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.Picha: Rouzbeh Fouladi/ZUMA/picture alliance

Rais Ebrahim Raisi wa Iran alitowa onyo hilo kali siku ya Ijumaa (Januari 2), akisema licha ya nchi yake kutokuwa muanzilishi wa vita vyovyote vile, lakini haitaliwacha taifa lolote jengine kuichezea Jamhuri ya Kiislamu na ikitokezea hivyo, basi Tehran itajibu kwa nguvu zote.

"Nguvu zetu za kijeshi kwenye ukanda huu hazikuwahi na bado si kitisho kwa nchi yoyote ile, bali chanzo cha usalama kinachoweza kutegemewa na kuaminiwa na nchi za ukanda huu. Hivi leo, adui hana uwezo wa kutufanya chochote, kwa kuwa anajuwa kuwa vikosi vyetu vina nguvu na vina uwezo." Alisema hayo akiwa kwenye kituo cha jeshi cha Bandar Abbas.

Soma zaidi: Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya shambulizi kubwa tangu mapinduzi ya mwaka 1979

Vifo vya wanajeshi wa Kimarekani kwa mashambulizi ya droni kwenye kituo kimoja cha kijeshi nchini Jordan siku ya Jumapili yalikuwa ya kwanza kabisa kwa Marekani kupoteza wanajeshi wake katika mashambulizi yanayoendelea kusambaa kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, tangu vianze vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, vilivyochochewa na mashambulizi ya kundi la Hamas ya tarehe 7 Oktoba.

Biden kuchukuwa hatua

Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye siku ya Ijumaa aliungana na familia za wanajeshi hao kuipokea miili na kutoa heshima zake kwao, ameyatuhumu waziwazi makundi yanayoungwa mkono na Iran kwa mashambulizi hayo. 

Rais Joe Biden wa Marekani.
Rais Joe Biden wa Marekani.Picha: Jonathan Ernst/Pool/File Photo/REUTERS

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari ameshaamua aina ya majibu yatakayotolewa na Marekani, lakini hajaweza wazi mpango wake hadharani, ama hata muda ambao atautekeleza, huku akisisitiza kwamba hana haja ya kuingia vitani moja kwa moja kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Ikulu ya White House imeonya kuwa hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa kujibu mashambulizi hayo.

Soma zaidi: Vita vya Gaza: Blinken afanya mazungumzo na Netanyahu

Muda wote, Iran imekuwa ikikanusha kuwa na mafungamano yoyote na mashambulizi hayo na imesema nayo pia haina nia ya kuutanuwa zaidi mzozo wa Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa wasiwasi umetanda kote kwenye eneo hilo tangu vita vya Israel na kundi la Hamas kuyavuta makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria, Iraq, Lebanon na Yemen.

Daima Jamhuri hiyo ya Kiislamu imekuwa ikisema kwamba ni wajibu wake kuyaunga mkono makundi inayoyaita ya wanamapambano kwenye ukanda huo, huku ikisisitiza kuwa makundi hayo yanafanya maamuzi na kuchukuwa hatua zake yenyewe.

AFP, AP