1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Erdogan na Netanyahu wakutana tangu mahusiano kuingia doa

20 Septemba 2023

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamekutana kwa mara ya kwanza na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana.

https://p.dw.com/p/4WZxC
Waandamanaji wa Kituruki wakichoma mfano wa bendera ya Israel
Mzozo wa Israel na Palestina umechochea kuzorota kwa mahusiano kati ya Israel na Uturuki Picha: AP

Mkutano wao unatajwa kuwa hatua ya kihistoria katika wakati mataifa hayo mawili yanajikongoja kuimarisha tena mahusiano yao.

Taarifa kuhusu mkutano huo uliofanyika mjini New York zinasema, viongozi hao wamejadili masuala ya kisiasa, uchumi na usalama wa kikanda ikiwemo mzozo wa Israeli na Palestina. Erdogan amemweleza Netanyahu kwamba nchi zao zinaweza kushirikiana kwenye maeneo ya nishati, teknolojia na uvumbuzi.

Nchi hizo mbili zilizowahi kuwa marafiki wa karibu, lakini zilitumbukia kwenye msuguano kiasi muongo mmoja uliopita ulioshuhudia Uturuki ikimtimua balozi wa Israel mnamo mwaka 2010.

Uamuzi huo ulifikiwa baada Israel kuuvamia msafara wa meli uliokuwa umebeba misaada ya kiutu kwenda Ukanda wa Gaza, kisa kilichosababisha vifo vya raia 10 wa Uturuki.

Mahusiano  yalirejea tena mwaka 2016 lakini miaka miwili baadaye Uturuki iliwarejesha nyumbani wanadiplomasia wake na kuwafukuza wale wa Israel pale vikosi vya Israel vilipowaua Wapalestina kadhaa walioshiriki maandamano huko Ukanda wa Gaza.