1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUturuki

Erdogan atangaza hali ya dharura katika maeneo ya tetemeko

Bruce Amani
7 Februari 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza hali ya dharura katika mikoa 10 iliyotikiswa na matetemeko mawili ya ardhi ambayo yamewauwa Zaidi ya watu 5,100 nchini Uturuki na Syria

https://p.dw.com/p/4NC7i
Syrien Jindayris Erdbeben Mann Trauer
Picha: Aaref Watad/AFP

Siku moja baada ya matetemeko hayo kutikisa Uturuki na Syria, waokoaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu wanapambana kuwaondoa watu kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Hali ya hewa ya baridi kali imeathiri juhudi za uokozi na upelekaji misaada, na baadhi ya maeneo hayana nishati.

Soma pia: Idadi ya vifo vya tetemeko la Uturuki, Syria yafikia 5,000

Katika hotuba yake leo, Rais Erdogan amesema mikoa 10 ya nchini Uturuki imeathirika kama eneo la mkasa huo na akatangaza hali ya dharura katika jimbo hilo kwa miezi mitatu. "kwa sasa, tuna vifo vya watu 3,549 na majeruhi 22,168. Faraja yetu kubwa ni kuwa zaidi ya raia wetu 8,000 wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi mpaka sasa."

Erdogan ambaye anakabiliwa na uchaguzi wa kitaifa katika miezi mitatu ijayo amesema serikali inapanga kufungua mahoteli katika mji wa kitalii wa Antalya, katika upande wa magharibi, ili kuwahifadhi kwa muda watu walioathirika na matetemeko hayo. "Tumepokea ahadi za msaada kutoka nchi 70 na mashirika 14 ya kimataifa. Tumezungumza na wakuu 18 wa nchi na serikali ambao" wametupigia simu.

Türkei | Besuch Präsident Erdogan im Notfallkoordinationszentrum in Ankara
Erdogan ametangaza hali ya dharura Picha: Depo Photos/ABACA/picture alliance

Hii itamruhusu rais na baraza lake la mawaziri kutohitaji idhini ya bunge katika kuweka sheria mpya na kuweka kikomo au kusimamisha haki na uhuru wa watu.

Nchini Syria, idadi ya vifo imefikia watu Zaidi ya 1,600, kwa mujibu wa serikali na idara ya uokozi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kaskazini magharibi.

Timu za uokozi kutoka karibu nchi 30 kote ulimwenguni zinaelekea Uturuki au Syria. Wakati ahadi za msaada zikiendelea kumiminika, Uturuki imesema itayaruhusu tu magari yaliyobeba misaada kuingia katika mikoa iliyoathirika kabisa ya Kahramanmaras, Adiyaman na Hatay ili kuharakisha shughuli za utafutaji na uokozi.

Soma pia: Jumuiya ya kimataifa yatoa mshikamano kwa Uturuki na Syria

Umoja wa Mataifa umesema unatafakari mbinu zote za kufikisha msaada kaskazini magharibi mwa Syria, ambako mamilioni ya watu wanaishi katika kiwango kikubwa cha umaskini na hutegemea msaada wa kiutu ili kuishi.

Umoja wa Ulaya umetuma timu 27 za uokozi kutoka nchi 19 kusaidia kuwatafuta manusura nchini Uturuki. Vitengo hivyo vinajumuisha wafanyakazi 1,150 wa uokozi na mbwa 70. Hii leo, Australia na New Zealand ni miongoni mwa nchi za karibuni kabisa kuahidi msaada nchini Uturuki na Syria.

Afp, ap, reuters, dpa