1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBurundi

Burundi yaomba msaada wa haraka kufuatia mafuriko

17 Aprili 2024

Serikali ya Burundi kwa ushirikiano na Umoja wa mataifa imetowa wito wa kupatiwa msaada wa haraka ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/4etPB
Mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, umeathirika na mvua nyingi zinazonyesha tangu mwezi septemba mwaka jana
Mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, umeathirika na mvua nyingi zinazonyesha tangu mwezi septemba mwaka jana Picha: artifant/blickwinkel/picture alliance

Hapo ni katika mtaa wa Kibenga Rural ulio kwenye ukingo za ziwa Tanganyika tuliko shuhudia wakaazi wakiokoa baadhi ya vitu vya matumizi ya ndani ya majumba, kufuatia maji kuzidi kuongezeka, ambapo tayari majumba mengi yamefunikwa na maji.

Patrick Nshimirimana Mkaazi wa eneo hilo ambaye maji tayari yamevamia sehemu ya nyuma ya nyumba yake anasema wanajianda kuondoka kwani maji kila kukicha yanazidi kuongezeka.

''Nyumba zinazidi kuharibika, Nyumba nyingi hapa tayari zimedidimizwa na maji ya ziwa. Tunaongeza mchanga tuone kama tutaendelea kuishi hapa. Tulitaraji kuwa Mvua zitapungua na maji ya Tanganyika kupungua lakini mvua zinaendelea kunyesha na Maji ya ziwa kuzidi kuongezeka. Ndio sababu lazima tuondoke hakuna njia mbadala''

Mgahawa maarufu kwa starehe na sherehe za harusi unao tambulika kama Safi beach tayari umefurika  maji ya ziwa. Manirambona Omar Mmiliki wa mgahawa huo anasema shuhuli zote zimesimama na wafanyakazi wake zaidi ya 60 wamesalia sasa bila ajira.

Kwenye kwenye barabara inayoelekea hadi Gatumba raia mwengine ameiambaia DW kuwa, alishuhudia hivi majuzi mwenziwe akiliwa na kiboko baada ya kuingia katika maji.

''Shule zote na zahanati zimefungwa''

Miundombinu kadhaa zimeharibika kutokana na mafuriko
Miundombinu kadhaa zimeharibika kutokana na mafurikoPicha: Ute Grabowsky/photothek/IMAGO

Gavana wa mkoa wa Bujumbura vijijini Desire Nsengiyumva amesema watu 7 wamepoteza maisha baada ya kuliwa  na kiboko na wanyama wengine, na kwamba zoni za Rukaramo na Gatumba kwenye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ndio ziloathiriwa zaidi. Na kwamba inafanyika sensa ili waweze kuhamishiwa katika maeneo yaliyo salama.

''Mitaa hiyo huvamiwa na maji kutoka ziwa Tanganyika na yale ya mto Rusizi, Nyumba elf 6 zimekwisha vamiwa na maji, na elfu 2 kubomoka kabisa. Waloathirika wako katika tabaka 3, wamiliki wa majumba, wapangaji na wengine ambao ni masikini. Tayari watu 1300 wameorodhesha, shule zote na zahanati zimefungwa''

Katika Tamko la pamoja la waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Martin Niteretse na msimamizi wa matawi ya Umoja wa mataifa nchini humo bi Violette Kakyoma wametowa wito wa msaada wa haraka ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Na kwamba watu zaidi ya laki 3 wanahitaji misaada huku wakisema makadirio ya hali ya hewa yanaonesha kuwa mvua bado zitaendelea kunyesha na Burundi ni miongoni mwa nchi 20 duniani zinazo zinazoshuhudia athari ya mabadiliko ya tabia nchi.