1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Uvamizi wa Urusi Ukraine unamhusu kila raia wa Ulaya

Jacob Safari
22 Februari 2023

Waukraine wameshuhudia uhalifu tangu Urusi ianze uvamizi mwaka uliopita. Waandishi wana jukumu la kusema ukweli wa mauti, uharibifu na matumaini ya Waukraine, anasema Mhariri mkuu wa DW, Manuela Kasper-Claridge.

https://p.dw.com/p/4NquX
Ukraine Krieg | Bachmut
Picha: Marek M. Berezowski/AA/picture alliance

Mamilioni ya Waukraine wameshuhudia uhalifu utokanao na vita tangu Urusi ianze uvamizi vmwaka mmoja uliopita. Waandishi wa habari wana jukumu la kumwambia kila mmoja ukweli wa mauti yanayofanyika, uharibifu na matumaini yasiyokufa ya Waukraine, anasema Manuela Kasper-Claridge Mhariri mkuu wa DW.

Theluji iliyo na damu inauzunguka mji wa Bakhmut. Kwa miezi sasa Urusi imejaribu kuuteka mji huu mdogo ulioko mashariki mwa Ukraine. Wameshambulia kutoka kila upande wakiungwa mkono na mamluki wa Wagner. Majumba na mitaa imedondoshewa mabomu bila huruma pasipo kujali vifo vya raia.

Kabla Urusi kuanzisha vita Bakhmut ulikuwa mji unaoishi watu 70,000 ila waliosalia kwa sasa hakuna anayefahamu. Ila waliosalia hawafi moyo, majeshi ya Ukraine yanaendelea kupigania uhuru wao kwa kuwa hawataki kuiachia Bakhmut kwa adui. Mji huu mdogo ni ishara ya upinzani wa Ukraine na ujasiri uliotokana na kukata matumaini.

Manuela Kasper-Claridge
Mhariri Mkuu wa DW Manuela-Kasper ClaridgePicha: Stephanie Englert/DW

Waandishi hawastahili kuficha ukweli

Na kinachotokea Bakhmut kinatuhusu sote, hatuwezi kufumba macho kwa yanayotokea katika udongo wa Ulaya, Kuna mauaji, mateso na ubakaji. Vita hivi si nadharia, katika vita kuna vifo na raia ambao ni wahanga na haya yanafanyika katika miji ya Bakhmut, Bucha, Irpin na Mariupol.

Kama waandishi wa habari tuna jukumu la kuripoti kuhusu unyama huu ila tunastahili kuchagua kwa makini cha kuonyesha. Hatuwezi kuficha ukweli ila tunastahili kuilinda heshima ya wahanga.

Bila shaka tunaripoti pia kuhusiana na jinsi raia wanavyokabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara katika uwanja wa vita. Jinsi wanavyokabiliana na maisha ambayo ni tofauti kwao na wakati huo huo wakiwa bado wana furaha na nguvu.

Ukweli ni upi na uongo ni upi? Si rahisi kusema hasa katika vita. Waandishi wetu wanaofanya kazi Ukraine wana mojawapo ya kazi ngumu zaidi. Wanastahili kushirikiana na wenzao kuhakikisha kwamba picha na kanda za video ni za kweli, wazungumze na mashuhuda na kufichua taarifa za uongo. Wanafanya yote haya wakiwa wanaishi katika hatari ya kuwa wahanga wa vita wao wenyewe.

Kazi hii ya kuripoti ni muhimu sana na madikteta wanahofia hasa aina hii ya uandishi huru wa habari.

Na ndio maana Rais Vladimir Putin anajaribu kutumia kila njia ya upotoshaji kuzuia ukweli kuhusu vita vya Urusi kuchapishwa. Anachotaka ni kwamba dunia au hata raia wake wenyewe wasijue kinachoendelea Ukraine. Anataka pia isijulikane ni raia wangapi waliouwawa kutokana na uvamizi wake au hasara iliyopata jeshi lake. Ukimya, kuficha na uongo ndiyo mambo anayotumia kuficha yale ambayo hayaingiliani vyema na propaganda zake.

Urusi na Propaganda zake

Ni vigumu kuzishinda propaganda za Urusi na kuwarudisha watu katiuka ukweli wa kinachoendelea ila kila juhudi ni muhimu. Ukweli unahitaji kujitokeza. Waandishi wa DW na wenzetu kutoka mashirika mengine wanajiweka sana katika hatari kuhakikisha kwamba ukweli unajulikana.

Moskau Rede Präsident Putin an Nation
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Metzel/Sputnik/AP/picture alliance

Wanavyofanya hivyo wanapokea uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa raia wa Ukraine. Wanataka ulimwengu ujue jinsi uvamizi wa Urusi unavyogharimu nchi yao na jinsi wanavyojilinda. Wanataka ijulikane pia kwamba kuna upinzani dhidi ya majeshi ya Urusi katika baadhi ya sehemu za Ukraine walizozikalia na kwamba kuna uhalifu dhidi ya binadamu unaofanywa na majeshi hayo ya Urusi.

Ripoti kama hizo hazionyeshwi katika vyombo vya habari vya kitaifa nchini Urusi. Vita hivi ni mapambano ya ukweli na udhibiti wa nadharia.

Kwa watu wengi, mwaka mmoja wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unamaanisha mapambano ya uhuru kwa Waukraine na kuilinda nchi yao. Mapambano haya yanastahili kuungwa mkono na kila raia wa Ulaya.

Kwa upande wetu sisi waandishi tunatoa taarifa zisizoegemea upande wowote, hiyo ndiyo kazi yetu. Tunaangazia yanayotokea nyuma ya pazia, kutoa muktadha na kuwa wazi kwa jinsi tunavyopata taarifa zetu ilia wafuatiliaji wetu wawe na maoni yao wenyewe kuhusiana na hali ya Bakhmut na nchi nzima ya Ukraine kuhusiana na ukweli na propaganda.

Mwandishi: Manuela Kasper-Claridge